#SheriaYaLeo (116/366); Chukua Hatua Kwa Ujasiri.
Wengi wetu huwa ni waoga.
Tunapenda kuepuka mivutano na migogoro na tunataka kukubalika na wote.
Tunaweza kufikiria kufanya jambo la kijasiri, lakini huwa vigumu kutekeleza.
Huwa tunaficha woga wetu kwa kujiambia tunajali wengine na hatutaki kuwaumiza.
Lakini huo siyo ukweli, tunachohofia zaidi ni wengine watatuchukuliaje.
Kwa kifupi woga ni ubinafsi.
Kwa upande mwingine ujasiri ni uwazi na kutokufikiria wengine wanakuchukuliaje.
Ujasiri ni kufanya kile kilicho sahihi na siyo kile ambacho kitawafurahisha wengine.
Kila mtu anapenda kuwa karibu na mtu jasiri, hata kama anachofanya hakina manufaa kwake.
Hiyo ni kwa sababu ujasiri unaambikizwa, unapokuwa karibu na mtu jasiri na wewe pia unapata ujasiri.
Hakuna aliyezaliwa jasiri, ni tabia ambayo mtu anajijengea kwenye maisha kama zilivyo tabia nyingine.
Kadhalika hakuna anayezaliwa mwoga, ni tabia inayojengwa.
Anza sasa kujijengea na kukomaza tabia ya ujasiri.
Kwa kila jambo unalopanga kufanya, lifanye kwa ujasiri mkubwa.
Weka pembeni woga na wasiwasi wowote ule.
Uzuri ni kwenye maisha kuna fursa mbalimbali za kuonyesha ujasiri.
Kwenye majadiliano, kwenye mauzo na kwenye ushawishi wa aina yoyote ile, kadiri unavyokuwa jasiri ndivyo unajiweka kwenye nafasi ya kupata kile unachotaka.
Kuwa na matakwa makubwa kwa kadiri unavyotaka wewe na kuwa jasiri kuyasimamia.
Usijali sana wengine wanakuchukuliaje, wengi hawakuchukulii vibaya kama unavyodhani.
Badala yake wengi wanakubali na kuvutiwa na ujasiri wako.
Kama woga umekutawala ni wakati wa kuuondoa kabisa.
Hofu yako kuhusu madhara ya hatua za kijasiri unazopaswa kuchukua haina nguvu.
Madhara ya woga ni makubwa na mabaya kuliko madhara ya ujasiri.
Woga unafanya udharauliwe na usikubalike, hakuna atakayekuwa tayari kukupa kile unachotaka.
Unapaswa kuwa jasiri na hata kama watu hawatakupa unachotaka, basi watakuheshimu.
Sheria ya leo; Woga ni hatari kubwa sana. Chukua hatua kwa ujasiri mkubwa. Makosa utakayoyafanya kwa kuwa jasiri, utaweza kuyatatua kwa kutumia ujasiri zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji