#SheriaYaLeo (117/366); Yafanye mafanikio yako yaonekane siyo ya juhudi kubwa.
Sisi binadamu huwa tunavutiwa na mafanikio ya watu wengine.
Huwa tunakubali pale mtu anapoweja juhudi na kupata mafanikio makubwa.
Lakini inapotokea mtu amepata mafanikio makubwa bila kuonekana akiweka juhudi kubwa, tunamkubali zaidi.
Tunaona ana uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee.
Tunamuona siyo mtu wa kawaida, kwa sababu kinachotusumbua sisi, yeye anafanya kwa urahisi.
Kumbuka siyo kwamba mtu huyo haweki juhudi, bali juhudi anazoweka hazionekani hadharani, anakuwa amezificha.
Hicho ndiyo unachopaswa kufanya pia, ficha juhudi zako na wafanye watu wayaone matokeo ya mwisho.
Wapo watakaotaka kujua umewezaje kukamilisha matokeo hayo makubwa, siyo lazima uwaambie au uwaonyeshe kila hatua.
Kwenye zama hizi za mitandao ya kijamii watu wanakwenda sana kinyume na hili.
Wanapenda kuweka kila juhudi zao wazi na kujigamba kwa namna wanaweka juhudi.
Haishangazi kwa nini kile wanachofanya hakithaminiwi.
Kwa sababu watu wanakiona ni cha kawaida.
Watu wasipoona juhudi unazoweka wanaona matokeo unayopata siyo ya kawaida, hivyo wanayathamini zaidi.
Sheria ya leo; Hatua unazochukua zinapaswa kuonekana za asili na rahisi kabisa kwako. Kwa kila unachofanya, fanya kwa namna ambayo unaonekana ungeweza kufanya zaidi. Epuka tamaa ya kutaka kuonyesha juhudi unazoweka kwenye kile unachofanya, inafanya watu wasikithamini sana.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji