2614; Mafuta na breki.
Ukiwasha gari na kukanyaga mafuta na breki kwa wakati mmoja, gari haiendi popote.
Itapiga kelele nyingi, mafuta yatatumika, lakini gari haitasogea hata hatua moja.
Lakini ukiondoa tu mguu kwenye breki, gari inakwenda mbele kwa kasi kubwa.
Hii ndiyo hali ambayo wengi wanakutana nayo kwenye safari ya mafanikio.
Wanaweka juhudi kubwa sana kwenye kile wanachofanya, lakini bado wanakuwa hawapigi hatua yoyote ile.
Wanaweza kuona kama wana bahati mbaya au kuna kitu hakipo sawa kwao.
Lakini ukweli ni kuba breki wameshikilia ndiyo maana juhudi wanazoweka haziwasukumi kwenda mbele.
Na breki za wengi zipo kwenye fikra, mtazamo, maono, tabia na mazingira.
Unapokuwa na fikra finyu, hakuna juhudi zitakazoweza kusaidia.
Kadhalika mtazamo hasi utakufanya uone mambo hayawezekani, hivyo juhudi unazoweka haziwezi kuleta matokeo makubwa.
Maono ndiyo dira yako kuu, bila maono utahangaika na mambo mengi yasiyo na tija. Hivyo japo utaweka juhudi sana, hakuna hatua ambazo utapiga.
Tabia ni kama ngozi, huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga. Mambo mengi unayofanya yanaongozwa na tabia, hivyo tabia zisipokuwa sahihi, juhudi unazoweka zinapotea bure.
Na mazingira yana nguvu kubwa sana. Kuanzia pale ulipo, kile unachofanya na watu wanaokuzunguka, vyote vinaweza kuwa kikwazo kikubwa.
Hasa wale wanaokuzunguka, kama nao hawapigi hatua, ni vigumu sana wewe ukapiga hatua.
Hatua ya kuchukua;
Pima juhudi unazoweka na matokeo unayopata, je vinaendana.
Kama haviendani jua kuna mahali umeweka breki.
Anza kuangalia kwenye kile eneo ili uone ni breki zipi umejiwekea wewe mwenyewe.
Bila kuondoa breki hizo, juhudi unazoweka utaishia kuzipoteza bure.
Tafakari;
Kitu kilichopo kwenye mwendo huwa kinaendelea na mwendo mpaka pale nguvu ya nje inapozuia mwendo huo. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio, kama husongi mbele, kuna nguvu inayokuzuia. Bila kuondoa nguvu hiyo, utapoteza jitihada nyingi sana.
Kocha.