#SheriaYaLeo (118/366); Epuka vitu vya bure.

Epuka sana vitu unavyopewa na wengine bure, kwa sababu huwa vina mtego wa kukunasa uwe mtumwa kwao.

Watu wanaokupa au kukufanyia vitu bure bila kudai malipo yoyote, baadaye huja na matakwa makubwa kwako ambayo yanazidi hata fedha ambayo ungewalipa.

Wengine kwa kukusaidia watatumia hilo kama njia ya kukunyanyasa kila wakati, uwasujudie wao kwa kile ambacho wamekusaidia.

Chochote unachopewa au kufanyiwa bure, kuna gharama zimejificha nyuma yake, ambazo lazima utazilipa tu.

Kwenye safari ya mafanikio, jua kila kitu kina gharama na unapaswa kulipa gharama hizo ili kufanikiwa.
Unapolipa gharama, unakuwa huru, hakuna anayekumiliki kwa namna yoyote ile.

Chochote chenye thamani kinapaswa kulipiwa, tena kulipiwa gharama yake kamili.
Hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio.
Gharama yoyote unayokwepa kulipa sasa, itakuja kukukamata baadaye na kuwa kikwazo kikubwa kwako.

Sheria ya leo; Jua kila kitu kina gharama zake na jifunze kulipa gharama hizo kwa ukamilifu wake ili uwe huru.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji