2615; Kazi ngumu ya uongozi.

Uongozi kwa nje huwa unaonekana ni mzuri na rahisi na hata watu kuvutiwa kuwa viongozi.

Viongozi wazuri na wabaya huonekana haraka kwa nje na watu kujilinganisha na viongozi hao na kuona wanaweza kuwa viongozi wazuri.

Ni mpaka pale mtu anapopata nafasi ya uongozi, hata kama ni mdogo kiasi gani ndipo anagundua kazi ngumu ya uongozi iko wapi.

Kazi ngumu ya uongizi ipo kwenye kufanya maamuzi magumu.

Na ugumu wa maamuzi hayo hautokani na kutokujua kipi cha kufanya, bali unatokana na madhara ya kila unachoweza kufanya.

Kwa nje unaweza kuona kwa urahisi nini kinapaswa kufanywa kwenye kila jambo.
Ndiyo maana wasio viongozi huwa wapo haraka kusema kiongozi angefanya hivi au vile.

Lakini kwa kiongozi mambo siyo rahisi hivyo, kwa kila chaguo alilo nalo, kuna faida na hasara zake.
Kwa kila maamuzi anayoweza kufanya, kuna madhara yatakayotokea.

Kazi hiyo inakuwa ngumu zaidi kwa sababu ni kiongozi peke yake ndiye anayepaswa kufanya maamuzi ya mwisho.
Pamoja na kuwa na washauri ambao watampa taarifa nyingi kuhusu hali husika, mwisho wa siku yeye ndiye wa kufanya maamuzi ya mwisho.

Na kwa maamuzi yoyote atakayofanya, lawama zitakuja kwake. Hakuna atakayejua kuhusu washauri wake au mwingine yoyote aliyemshawishi kufanya maamuzi hayo.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye maisha yako, jijenge kuwa kiongozi bora kwa kila hatua unayopitia kwenye maisha yako.
Kabili changamoto ngumu zinazohitaji maamuzi magumu.
Jikengee misingi utakayokuwa unaisimamia kila wakati wa kufanya maamuzi.
Na miliki matokeo ya kila maamuzi unayoyafanya, bila kujaribu kuyakimbia, kuyakwepa au kulaumu wengine.

Tafakari;
Ni rahisi kuona uongozi ni rahisi kama haupo kwenye uongozi.
Ni rahisi kuona maamuzi ya kufanya pale unapokuwa siye unayewajibika kwa maamuzi hayo.
Uongozi siyo rahisi kama unavyoonekana kwa nje.
Ndiyo maana viongozi wazuri ni wachache.

Kocha.