2617; Kwenye uzio.
Huingii ndani na wala hutoki nje.
Hiyo ni hali ambayo wengi wamekuwa wakijikuta hasa wanapohitajika kufanya maamuzi.
Na hilo ndiyo limekuwa linafanya wengi wasubiri mpaka tarehe ya mwisho (deadline) ndiyo wafanye kitu.
Kukaa kwenye uzio hakujawahi kuwa na manufaa, zaidi ya kumpotezea muda.
Utaona unapata muda zaidi wa kupata taarifa zaidi, lakini kiuhalisia ni unapoteza muda kwa kutokufanya maamuzi.
Amua kuingia ndani au kutoka nje, utaokoa muda wako na kuweza kufanya mengi.
Haimaanishi ukimbilie kufanya maamuzi kama hujawa tayari.
Bali hupaswi kuzunguka na maamuzi kwa muda mrefu bila kuamua.
Na inapokuja kwa wengine unaotaka wafanye maamuzi fulani, wape sababu ya kufanya maamuzi mara moja kuliko kukaa kwenye uzio.
Ni bora mtu akuambie hapana ujue umemkosa kuliko aendelee kukusubirisha bila jibu.
Maana utatumia kwake muda na rasilimali nyingi ambazo huwezi kuzitumia kwa wengine.
Hatua ya kuchukua;
Unapojikuta kwenye hali ya kushindwa kufanya maamuzi, huku maamuzi hayo yakikufikirisha kwa muda mrefu, amua kuchagua chochote na kwenda nacho. Kama haitakuwa sahihi utabadili.
Unapotaka wengine wafanye maamuzi, wape sababu ya kufanya maamuzi sasa na siyo kuendelea kusubiri.
Tafakari;
Unaweza kuona ni raha kukaa kwenye uzio, kwa sababu unakuwa hujajitoa kikamilifu kwenye upande wowote.
Lakini raha kamili ipo kwenye kufanya maamuzi na kuyasimamia.
Hata kama utakuwa umefanya maamuzi mabovu, utajifunza mengi kuliko kutokufanya maamuzi kabisa.
Kocha.