#SheriaYaLeo (124/366); Wahukumu kwa tabia zao, siyo maneno yao.
Kwenye safari yako ya mafanikio na maisha kwa ujumla, jifunze kutokudanganyika na maneno ambayo watu wanakuambia, badala yake angalia tabia wanazokuonyesha.
Watu husema maneno ya kila aina na kujaribu kuficha nia zao halisi kwa maneno mazuri.
Lakini matendo yao huwa hayadanganyi, huwa yanaweka wazi nia zao halisi.
Kwa kifupi maneno yanadanganya lakini matendo yanaweka kila kitu wazi kabisa.
Hivyo pale maneno na vitendo vya mtu vinapokinzana, amini zaidi vitendo kuliko maneno.
Kwa maneno mtu anaweza kujinadi ni mwema na anayejali.
Lakini kama vitendo vyake vinaonyesha mtu huyo ni muovu na asiyejali, huo ndiyo ukweli wake.
Mara nyingi watu hutumia maneno na maigizo ya nje kuficha nia zao halisi ili kuwahadaa watu waweze kupata kile wanachotaka.
Wajibu wako ni kuhakikisha huhadaiki na maneno au maigizo yao.
Waangalie kwa makini zaidi watu pale wanapokuwa kwenye hali zisizo za kawaida kwao.
Mfano wanaokuwa na msongo au hasira.
Katika hali za aina hiyo hawawezi kuingiza, tabia zao halisi zinakuwa hadharani.
Hivyo amini zaidi yale watu wanayoyaonyesha wakiwa kwenye hali ngumu kuliko wanayoyaonyesha wakiwa kwenye utulivu.
Lakini pia tabia ambayo watu wanatumia nguvu kubwa sana kuionyesha kwa nje, ndani yao ni kinyume kabisa.
Wale wanaojisifu na kujigamba, ndani yao hawajiamini.
Wanaojipendekeza sana kama marafiki wanaojali, ndani ni maadui wenye nia mbaya.
Jifunze kuona zaidi ya kile ambacho watu wanaigiza.
Weka umakini mkubwa kwenye ambayo watu wanafanya na siyo wanayosema au kuigiza.
Usipuuze chochote ambacho watu wanaonyesha, kitu kidogo kinaweza kuwa na maana kubwa.
Sheria ya leo; Unachohitaji ni picha ya tabia halisi ya mtu, ambayo itakuchukua muda kuipata kwa ukamilifu. Epuka mazoea ya kuhukumu watu haraka kwa maneno au mwonekano wa nje. Jipe muda kuzijua tabia halisi za watu na hapo ndiyo unaweza kuwajua kweli.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji