#SheriaYaLeo (128/366); Wanaotumia udhaifu kukutawala.
Kuna watu huwa wanatumia udhaifu walionao kukutawala wewe bila ya mwenyewe kujua.
Wanakuwa na tabia fulani sugu ambayo inakukwamisha wewe, lakini unapojaribu kuwakabili kwenye tabia hiyo wanajionyesha hawana hatia na wewe ni mtu mbaya na usiyejali.
Wanaweza kuwa na tabia sugu ya kuchelewa kila wakati.
Au kusahau vitu muhimu ambavyo mmekubaliana.
Kwa nje wanaonekana kutokuwa na hatia katika kufanya hayo.
Ila kwa ndani wanakuwa wanafanya makusudi kabisa.
Wanajua kwa yale wanayofanya lazima utakasirika na ukishakasirika utachukua hatua fulani dhidi yao na hapo sasa ndiyo watageuza kibao na kufanya ujione wewe ndiye mbaya.
Lengo lao ni kutumia hatia kukutawala wewe.
Pale unapowakabili kwa udhaifu wao wanajifanya hawana hatia na kuonyesha wewe ni mtu usiyejali.
Ni muhimu sana uwatambue watu wa aina hii kwenye maisha yako na kutokukubali wakutawale kwa udhaifu wao.
Ukishawatambua waeleze wazi unajua kile wanachofanya na hapo watakosa nguvu ya kuendelea na mbinu zao.
Na muhimu zaidi, mara zote simama kwenye kile kilicho sahihi na usikubali mtu akugeuzie kibao kwa makosa na uzembe wake mwenyewe.
Kama mtu amekwenda kinyume na utararibu basi apewe adhabu anayostahili bila ya kuruhusu mbinu zao za kujifanya hawana hatia zikuingie na kukufanya uone ni vibaya kuchukua hatua uliyopanga.
Sheria ya leo; Pale mtu anapokuwa na tabia sugu inayokukwamisha, hakikisha hufanyi jambo lolote kwa hasira, maana huo ndiyo mtego anaokuwa amekuwekea. Badala yake kuwa mtulivu na mweleze wazi unajua anachofanya na geuza aibu iwe kwake. Kwa njia hiyo mtu ataacha kutumia udhaifu wake kukutawala.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji