2625; Usife.

Katika safari ya mafanikio ya mtu yeyote yule, bahati ina mchango wake.

Kila historia ya aliyefanikiwa, kuna mahali alikutana na bahati au fursa ya kipekee na ikampa manufaa makubwa.

Kinachowatofautisha wanaokutana na bahati na ambao hawakutani nazo siyo bahati yenyewe, bali muda.

Yaani siyo kwamba kuna watu wana bahati na wengine hawana bahati.
Bahati imesambazwa sawa kwa wote.

Ila sasa, wengi wanakufa kabla hawajakutana na bahati zao.
Na hapa simaanishi kifo cha maisha, bali kifo cha safari.

Ni pale biashara ya mtu inapokufa mapema na hapo kukosa fursa nzuri za baadaye.

Ni pale mtu anapokata tamaa mapema na kuachana na safari yake ya mafanikio.

Sheria kuu ya kufuata kwenye maisha yako ni hii; usife.
Kwa chochote unachofanya, hakikisha unaendelea kukaa kwenye mchezo kwa muda mrefu iwezekanavyo.

Epuka sana kuchukua hatua ambazo zitakupeleka kwenye kifo, kwani huwezi kupambana ukiwa umekufa.

Mara zote hakikisha unabaki hai kwenye mchezo na safari ya mafanikio.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kukutana na bahati yako na kuweza kufanya makubwa.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila maamuzi unayofanya, hakikisha hayakuondoi kabisa kwenye mchezo. Usipate tamaa ya kupata sana ukachukua hatari ambayo ukipoteza unapoteza kila kitu.
Mara zote fanya maamuzi ambayo yanakupa nafasi ya kuendelea kufanya hata kama umepoteza.
Hiyo ndiyo njia ya kukukutanisha na bahati yako ambayo iko njiani ikija kwako.

Tafakari;
Charlie Munger amewahi kusema ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa ili nisiende hapo.
Huo ni ukweli muhimu, ukifa ndiyo mwisho, ukiwa hai una fursa nyingi mbele yako.

Kocha.