2626; Kujisumbua bure.

Kama kuna msingi mmoja muhimu wa kujifunza kwenye falsafa ya Ustoa ambao utafanya maisha yako yawe bora kabisa ni huu; kuna mambo yako ndani ya uwezo wako na mengine nje ya uwezo wako, hangaika na yaliyo ndani ya uwezo wako na achana na yaliyo nje ya uwezo wako.

Ukiangalia, matatizo makubwa tunayokutana nayo kwenye maisha yanatokana na kuhangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wetu.

Kuna vita inaendelea duniani, unatumia muda wako mwingi kufuatilia habari ili ujua kila kinachoendelea, je hilo lina nguvu ya kubadili chochote?

Unajisumbua bure kuhangaika na mambo ambayo huna namna ya kuyaathiri. Unachoka huku ukiwa hauna matokeo ya tofauti unayokuwa umesababisha.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila jambo linalokukabili, jiulize kama lipo ndani au nje ya uwezo wako. Kama unaweza kuchukua hatua na kuliathiri basi lipo ndani ya uwezo wako na chukua hatua hiyo. Kama kuchukua hatua hakuwezi kuathiri chochote lipo nje ya uwezo wako hivyo achana nalo.

Tafakari;
Kuhangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wako ni kujitesa bure, maana hakuna namna unaweza kuyabadili.
Yakubali kama yalivyo yale yaliyo nje ya uwezo wako na peleka nguvu zako zote kwenye yale yaliyo ndani ya uwezo wako.

Kocha.