#SheriaYaLeo (131/366); Usichanganye kujiamini kulikopitiliza na ukweli.

Sisi binadamu huwa tunadanganyika kirahisi sana.
Pale mtu anapotueleza kitu kwa kujiamini sana, huwa tunaona ni ukweli, kwamba kama isingekuwa kweli basi wasingejiamini.

Hii ndiyo njia wanayotumia matapeli na watu wengine wenye lengo la kudanganya na kuhadaa kwa manufaa yao.
Huwa wanaeleza jambo kwa kujiamini sana na kutumia mifano inayoshawishi, hata kama siyo ya kweli.

Unaweza kushangaa kwa nini pamoja na maendeleo ambayo binadamu tumepiga kwa ujumla, pamoja na wingi wa maarifa yanayopatikana kwa urahisi bado watu wanadanganyika.
Hiyo ni kwa sababu asili yetu binadamu haibadiliki kirahisi.
Bado tuna tabia ya kuwaamini watu kwa kile tunachoona na kusikia badala ya kuchunguza kwa ndani zaidi.

Jifunze kuzigundua dalili za uongo na utapeli mapema, ikiwepo watu kujiamini kupitiliza.
Pale mtu anapotumia nguvu nyingi kueleza au kutetea kitu, pata wasiwasi.

Ukweli huwa hauhitaji nguvu nyingi kutetewa. Huwa unabaki kuwa ukweli bila hata ya mbwembwe zozote.
Hivyo unapoona mbwembwe nyingi kwa mtu, jua kabisa kuna kitu anaficha.
Ni wajibu wako kuchunguza kwa ndani ili kujua ukweli kabla hujafanya maamuzi yoyote.

Sheria ya leo; Watu wanapojaribu kuelezea kitu kwa kutumia nguvu kubwa au kujitetea kwa kuonyesha kwamba hawana hatia na wanaonewa, huo ndiyo wakati wa kupata wasiwasi kwamba kuna kitu wanaficha. Usihadaike na kile wanachoonyesha, chunguza kujua ukweli.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji