2628; Ndiyo biashara yenyewe.

Sisi binadamu huwa tunafanya vitu kwa misukumo ya hisia mbili; tamaa na hofu.

Huwa tunafanya kitu kama kuna kitu kizuri tunapata (tamaa) au kama hatutaki kupoteza tulichonacho (hofu).

Kwa kujua hili, inakusaidia sana kuelewa kwa nini baadhi ya watu huwa wanafanya vitu ambavyo hukutegemea wafanye.

Unaweza kushangaa mtu anafanya mambo ya ajabu kabisa kwenye kazi au biashara yake.
Unaweza kujiuliza anawezaje kufanya mambo ya aina hiyo.

Jibu lipo wazi, mtu anafanya mambo hayo kwa sababu yanalipa.
Yanalipa kwa kumpa kile anachotaka au kuzuia asipoteze alichonacho.

Hata kama mambo hayo yana madhara baadaye, kwa sasa yanakuwa na manufaa kwa mtu.
Na kwa kuwa wengi huwa hawawezi kuangalia na kupima mambo ya baadaye, hawajisumbui na hilo.

Unapoona kitu kinafanywa na watu kwa kujirudia rudia na kwa muda mrefu, jua kinalipa.

Unapojiuliza mbona watu wanafanya mambo fulani kwenye biashara, jua ndiyo biashara yenyewe.

Chukua mfano wa ‘kiki’, yaani kutumia kasha au sifa nyingine mbaya kupata umaarufu.
Unaweza kujiuliza iweje watu wakubali kujiingiza kwenye mambo yanayowapa sifa mbaya.

Lakini ukweli ni kwamba wao wanachojali siyo sifa, bali ule umaarufu, kufuatiliwa na wengi.

Lengo lao ni taarifa ziwafikie wengi na kwa kuwa taarifa hasi husambaa kwa kasi kuliko chanya, lengo lao kinatimia haraka wakitumia sifa mbaya.

Kwa kujua hili, jikumbushe kila unapokutana na watu wanaofanya mambo ambayo hukutegemea wafanya, jua hawafanyi kwa kubahatisha, bali ndiyo mpango wenyewe.

Hatua ya kuchukua;
Usihangaike sana na yale ambayo watu wanafanya, kwani kuna namna yana manufaa kwao. Maana hakuna aliye timamu anayefanya kitu kisichokuwa na manufaa kabisa kwake.
Katika kujenga biashara au kingine chochote, tumia zaidi sifa nzuri ambapo unahitaji kazi na muda, kuliko sifa mbaya ambapo ni rahisi.

Tafakari;
Kwa asili sisi binadamu ni wa binafsi, kwa lolote tunalofanya, huwa tunaanza kujiangalia sisi wenyewe kwanza. Hivyo usishangae pale watu wanapofanya vitu fulani, jua vina manufaa fulani kwao.

Kocha.