#SheriaYaLeo (132/366); Angalia tabia wanazoficha.

Katika kuchagua watu wa kushirikiana nao, huwa tunaamini haraka kile ambacho tunasikia na kuona kwao.
Tunaamini hivyo ndivyo watu walivyo na yale wanayotuambia na kutuonyesha ndiyo uhalisia wao.

Tunachosahau ni kila mtu kuna tabia anazo ambazo huwa hapendi kuziweka wazi.
Huenda hata yeye mwenyewe hajui ana tabia za aina hiyo.

Utazijua tabia hizo kwa kuangalia historia ya mtu na kote ambapo ameshapita.
Angalia mahusiano yote ambayo amewahi kuwa nayo, kazi au biashara zote amewahi kufanya na maamuzi yote ambayo amewahi kufanya.

Kwa kufanya hivyo utaona mwendelezo fulani wa vitu kwa mtu ambao ndiyo tabia yake halisi.
Kuna namna anachukulia na kufanya vitu vyake ambayo ndiyo inamletea matokeo yote anayopata kwenye maisha yake.

Kamwe usipuuze hilo, maana litakuathiri pale utakaposhirikiana naye.
Usisikilize pale anapokuambia amebadilika, tabia ambayo mtu amekuwa nayo maisha yake yote huwa haibadiliki haraka.

Yote ambayo mtu anafanya kujinadi na kushawishi watu wakubaliane naye huwa yametengenezwa kwa machache ambayo mtu anajua yana ushawishi.
Ukitaka kumjua mtu vizuri, angalia tabia zake halisi za nyuma na siyo kusikiliza kile anachosema au kuonyesha.

Sheria ya leo; Puuza mwonekano ambao watu wanatengeneza na hadithi walizojenga juu yao. Badala yake angalia kwa kina tabia zao za nyuma. Angalia maamuzi ambayo wamewahi kufanya huko nyuma, jinsi wamekuwa wanashirikiana na wengine na matokeo ambayo amekuwa anapata. Historia ya mtu haidanganyi, maana ndiyo mtu mwenyewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji