2630; Udhaifu wako mwenyewe.

Matatizo na changamoto nyingi vimekuwa vinajirudia kwa watu, kwa sababu huwa hawakubali chanzo cha hayo.

Wao hukazana kutafuta wengine wa kulaumu isipokuwa wao.
Wanakuwa na ushahidi kabisa wa jinsi wengine wamehusika kwenye yale wanayopitia.

Lakini hata wanapomaliza hilo, bado mengine yanaibuka.
Hayakomi kwa sababu mtu anakimbilia kutafuta sababu za nje na kuficha udhaifu wa ndani yake mwenyewe.

Inakuwa rahisi mtu kuona madhaifu na makosa ya wengine kuliko kuona kwa upande wake.

Kuondokana na hilo na ili matatizo na changamoto zisijirudie, kwa kila unachopitia jiulize umekichangiaje.
Kwa kila tatizo au changamoto unazokabiliana nazo, jua kuna namna wewe mwenyewe umezitengeneza.

Hata kama ipo wazi kabisa kwamba wengine ndiyo wamefanya mambo fulani kusababisha changamoto zako.
Bado wewe mwenyewe kuna namna umechangia katika hilo.

Ukiweza kujihoji na kujua mchango wako kwenye kila kitu unachopitia, utaweza kuepuka mengine kabla hata hayajatokea.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila tatizo au changamoto unayopitia, swali la kwanza unalopaswa kujiulize ni umeisababishaje mwenyewe.
Jiulize ni udhaifu gani wa ndani yako ambao umepelekea tatizo hilo kutokea.
Kwa kuujua na kuufanyia kazi, utazuia hali kama hiyo isijirudie tena.

Tafakari;
Wanasema unapomnyooshea kidole kimoja mtu mwingine, vidole vitatu vinarudi kwako. Hiyo ina maana wewe unahusika zaidi kwenye jambo lolote kuliko yule unayemlaumu. Anza kufanyia kazi upande wako na utazuia mambo hayo yasijirudie.

Kocha.