#SheriaYaLeo (136/366); Zawadi za kimtego.

Watu wenye hila ya kupata kitu fulani, huwa wanapenda kuficha nia yao kwenye kitu kingine ili wasionekane waziwazi.

Moja ya maeneo ambayo watu wanaotaka kujinufaisha kupitia wengine ni utoaji zawadi.

Watu hao huwa wanatoa zawadi za kimtego.
Wanachofanya ni kumpa mtu zawadi ndogo, halafu baadaye wanakuja kuwataka wawape kitu kikubwa.

Sisi binadamu huwa ni dhaifu sana kwenye eneo la zawadi.
Tangu watoto tumezoea kwamba zawadi ni upendo, anayekupa zawadi basi anakupenda.

Hivyo hata yule mwenye hila mbaya anapotumia njia hiyo, tunasahau mengine yote na kuona ana upendo.
Hilo linafanya tusiwe na tahadhari na mwishowe tunaumia.

Kutoa kidogo na kuja kuomba kikubwa ni mbinu ya ushawishi ambayo imekuwepo tangu enzi na enzi.
Lakini bado huwa inatunasa kwa sababu ni vigumu sana kukataa zawadi na ukishapokea unajiona unawajibika kutoa.

Ni muhimu sana uzitambue zawadi unazopewa kama mtego wa mtu kuja kupata zaidi kupitia wewe.
Pale kunapokuwa hakuna sababu ya msingi ya mtu kukupa zawadi au hamna ukaribu wa kuhalalisha zawadi ni vyema kuepuka zawadi hizo.

Ukishazipokea tu zawadi za kimtego, unakuwa umenasa kwenye mtego wenyewe na ni vigumu sana kujinasua.
Ukishapokea, hata kama ni kidogo utajikuta unatoa sana.
Maana wanaokupa zawadi hizo wanajua jinsi ya kukubana ili wapate kila wanachotaka.
Salama yako ni kutokukubali kupokea zawadi hizo.

Sheria ya leo; Huwa tunaweza kuona matendo maovu ya watu kwa urahisi. Ila yanapofichwa nyuma ya zawadi, inakuwa vigumu kwetu kuona nia ovu. Kuwa makini sana na kila zawadi unayopewa, kuna ambazo zimekaa kimtego, zenye lengo la kuchukua zaidi kutoka kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji