#SheriaYaLeo (138/366); Tambua Kivuli Cha Watu.

Kwenye safari yako ya maisha utakutana na watu ambao wanatumia nguvu kubwa kuonyesha tabia fulani nzuri kwa nje.

Inaweza kuwa ni huruma iliyopitiliza, kujali sana, kuonekana watakatifu au imara sana.

Lakini pale unapowajua watu hao kwa undani, unaona kuna kivuli kipo nyuma ya tabia hizo wanazozionyesha.
Kivuli hicho kinakuwa ni tabia nyingine ambazo zipo kinyume kabisa na hizo wanazokazana kuonyesha.

Unapochunguza kwa undani ndiyo unajua uhalisia, ambao unaweza kutokana na mambo mawili.

Moja ni watu hao waliwahi kujeruhiwa mwanzoni kwenye maisha yao kutokana na tabia zao za kujali na hapo wakajifunza kuwa na tabia zitakazowalinda.

Mbili ni watu hao wanaweza kuwa na matamanio makubwa ambayo jamii inayowazunguka inayaona siyo sawa. Hivyo wanajenga tabia za kuficha matamanio yao makubwa ili wasikutane na vikwazo vya wengine.

Kwa miaka mingi watu wanakuwa wamejenga tabia na sifa fulani ya kuonekana kwa wengine, lakini ndani yao wanakuwa ni watu tofauti kabisa.

Sheria ya leo; Kuwa makini na watu wanaoonyesha tabia nzuri kupitiliza. Ni rahisi kunasa kwenye mtego wao wa mwonekano wa nje. Angalia mabadiliko yao ya tabia kadiri unavyowajua, hizo ndiyo zinakuwa tabia zao halisi. Usione kama wamebadilika, bali umewajua kwa undani zaidi na kutambua vivuli vyao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji