2635; Usidharau.
Naweza kusema matatizo yote makubwa tunayokutana nayo kwenye maisha, yanaanzia kwenye dharau.
Siyo tu ile dharau ya nje unayoweza kuonyesha kwa vitu au watu, bali zaidi ile dharau ya ndani inayofanya uone kitu siyo muhimu sana au hakina madhara makubwa.
Na dharau ipo kwenye mambo yote, mazuri na mabaya. Unaweza kudharau mambo mazuri na hilo likakuzuia kunufaika nayo.
Au unaweza kudharau mambo mabaya na yakakuumiza zaidi.
Unaweza kumwona mtu ni mjinga, ukadharau ujinga wake na hilo likaja kuleta madhara makubwa kwako kutokana na jambo la kijinga analokuja kufanya mtu huyo.
Ambapo kama usingedharau ujinga wake na kuona hakuna anachoweza kufanya, ungemzuia mapema na usingeingia kwenye matatizo uliyojikuta upo.
Hakuna eneo ambalo dharau ina madhara makubwa kama kwenye tabia.
Mambo madogo madogo, unayoyafanya kila siku kwa kujirudia rudia huwa ndiyo yanajenga maisha yako.
Wewe utayaona mambo hayo ni madogo na kuyadharau, lakini kitendo cha kuyarudia kila siku yanajenga nguvu kubwa baadaye.
Ukiyapitia maisha yako na kukumbuka mambo ambayo umeshayapitia mpaka sasa, utaona jinsi dharau kwenye mambo madogo zilivyoleta madhara makubwa kwenye maisha yako.
Utaona jinsi kukosa umakini kidogo tu kumeharibu mambo mengi mazuri.
Hatua ya kuchukua;
Kamwe usidharau kitu kidogo, iwe kwa nje wazi au ndani yako na iwe ni kizuri au kibaya.
Kila kitu kina nguvu ya kuleta madhara kwenye maisha yako.
Kabla ya kudharau kitu na kuona hakina nguvu, jiulize kama kitaendelea kwa ukubwa zaidi ya kilivyo sasa, matokeo yake yatakuwaje?
Hayo utakayoyaona ndiyo matokeo halisi kama utadharau.
Tafakari;
Matatizo huwa hayaanzi kwa ukubwa ambao una usumbufu kwa watu.
Bali huwa yanaanza kwa hatua ndogo kabisa, ambazo watu wanazidharau na hivyo yanapata fursa ya kukua zaidi.
Wahenga waliona haya mapema na kusema usipoziba ufa utajenga ukuta na pia mdharau mwiba mguu huota tende.
Bado hatujawa na akili kuwazidi wahenga, tuwasikilize.
Kocha.