2636; Furahia kupitwa.

Maamuzi yetu mengi huwa yanasukumwa na hofu ya kupitwa, ambayo kwa kiingereza inaitwa FOMO – Fear Of Missing Out.

Fuatilia mfano huu mfupi.

Wao; Aisee kuna fursa mpya imekuja, unapanda pesa zako mahali, halafu baada ya miezi mitatu unavuna mara mbili.

Wewe; Mh, hakuna kitu cha aina hiyo, lazima utakuwa ni utapeli. Tumeona vitu vingi vya aina hiyo na watu wakakaishia kupoteza.

Wao; Ndiyo tatizo lako, unazikosa fursa nzuri kwa sababu ya hofu tu. Kumbuka no risk no reward.
Halafu hii ni ya tofauti, siyo sawa na hizo ulizosikia.

Wewe; Zote zinakuwaga hivyo tu, na hata hivyo fedha zangu kwa sasa nimeweka kwenye biashara nyingine ambayo inachukua muda wangu mwingi.

Baada ya miezi mitatu…

Wao; Aisee tumetoka kuvuna tulichopanda, hebu ona faida kubwa tuliyopata.

Wewe; Acha bwana, kumbe hii kitu ni kweli?

Wao; Ni kweli kabisa na wewe tu ndiye unayepitwa.

Wewe; Hapana, sikubali kupitwa, natoa fedha kwenye biashara nipande huko kwa hiyo miezi mitatu, halafu nikishavuna faida narudisha mtaji kwenye biashara na naendelea kupanda faida.

Baada ya miezi mitatu.

Wewe; Aisee muda wa kuvuna tulichopanda umefika, mbona hatupati faida tuliyoambiwa.

Wao; Kuwa na subira, kuna mambo kidogo hayajakaa sawa, yakikaa sawa kila mtu atapata mavuno yake.

Miezi sita baadaye…

Wewe; Unawatafuta.

Wao; Hawapatikani.

Ndiyo unazinduka ‘umepigwa’, pesa umepoteza na biashara imekufa.
Mwanzo ulikuwa na msimamo mzuri, ambao ungekusaidia.
Lakini tamaa ya kupata ikakunasa kwa hofu ya kukosa na ukaingia kwenye kitu kisichokuwa sahihi.

Somo hapa ni nini?
Ukishachagua eneo unalokwenda kufanyia kazi ili kufanikiwa, furahia kabisa kukosa fursa nyingine.
Yaani watu wakija kwako na kujigamba na fursa nzuri zinazowalipa, furahia kwamba unazikosa fursa hizo ili kujenga kile kilicho muhimu kwako.

Ndiyo kwa msimamo huo utazikosa fursa nyingi nzuri, lakini pia utaepukana na utapeli mwingine mwingi.

Badala ya FOMO – Fear Of Missing Out unapaswa kuwa ba JOMO – Joy Of Missing Out.
Furahia kabisa kuzikosa fursa nzuri ambazo wengine wananufaika nazo, kwa sababu tayari wewe umeshachagua fursa yako kuu.
Hata kama fursa kuu uliyochagua haikulipi sana kwa sasa, usikate tamaa, juhudi unazoweka zitakuja kukulipa sana baadaye.

Hatua ya kuchukua;
Ukishajua kile unachotaka kwenye maisha yako na ukishachagua njia utakayotumia kukipata, acha kuhangaika na kila fursa inayokuja mbele yako.
Kila kitu ni rahisi na kizuri kwa kuelezwa na kukiona kwa nje.
Ni mpaka uingie ndani ndiyo utaona uhalisia wake.
Kwa sababu huna muda wa kujaribu kila kitu ili kujua usahihi wake ni vyema ukapuuza fursa nyingi zisizoendana na unachofanya.

Tafakari;
Fursa ni nyingi na hazitakuja kuisha.
Kila siku kuna fursa mpya na nzuri zinazokuja.
Ukiwa mtu wa kukimbizana na fursa mpya kila wakati, utaishia kutokufanya chochote kikubwa.
Tulia kwenye fursa moja mpaka izae matunda ya uhakika.

Kocha.