2637; Sahihi na siyo sahihi.
Mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema kipimo cha akili iliyokomaa ni kuweza kushikilia kwenye akili mawazo mawili yanayopingana kwa wakati mmoja.
Hili ni zoezi gumu mno kwa sababu kwa kawaida binadamu huwa tunapenda sana uhakika.
Kukaa na mawazo mawili yanayopingana ni kukosa uhakika.
Wengi huona ni bora wachague moja na kuliamini hata kama siyo sahihi kuliko kuendelea kujitesa na mawazo yote kwa wakati mmoja.
Na hii ndiyo maana watu hupenda kujiunga na itikadi fulani. Na wakishakuwa kwenye itikadi hizo, ni vigumu sana kuwashawishi kitu cha tofauti.
Tunaweza kusema akili ikishakubali itikadi basi inakuwa imepoteza uwezo wake mkubwa wa kuhoji na kudadisi mambo.
Kitu kikubwa unachopaswa kukijua na ambacho kitakusaidia sana kwenye safari yako ya mafanikio ni kila kitu ni sahihi na pia siyo sahihi. Hilo linaweza kuwa kwa wakati mmoja au kwa nyakati tofauti.
Hivyo badala ya kupoteza muda kutafuta kitu ambacho ni sahihi kabisa, tumia asilimia kufanya maamuzi.
Kwamba kwa kitu ni kwa asilimia ngapi ni sahihi na asilimia ngapi siyo sahihi?
Hilo litakusaidia kujua kuna nasafi ya kutokuwa sahihi au kukosea na hapo unapaswa kuwa na tahadhari kubwa.
Pia itakusaidia kuendelea kudadisi na kujifunza kwa kina kitu kinachofanya uwe bora zaidi.
Kujipa uhakika ambao haupo ni njia ya uhakika ya kwenda kwenye anguko.
Mara zote jipe nafasi ya kwamba haupo sahihi au unakosea, utakazana kufanya kwa ubora zaidi.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapojiambia una uhakika wa kitu, hapo hapo jikamate. Jiambie kuna kitu hakipo sahihi na hivyo anza kukitafuta au kuthibitisha kwamba hakipo.
Epuka sana kuingia kwenye itikadi yoyote ile, maana inakupa upofu, unayaona mazuri tu ila mabaya yaliyopo wazi huyaoni.
Tafakari;
Ukuaji wa sayansi umetokana na msingi wake mkuu wa kutilia mashaka na kuhoji kila kitu, hata kile ambacho kilishakubalika na kila mtu ni sahihi. Hapo ndipo makosa mengi yamekuwa yanayonekana na kuboreshwa na hatua kupigwa.
Kudumaa kwa dini kumetokana na kuamini kila kitu jinsi kilivyo bila ya kuhoji chochote. Kuona upande ambao mtu yupo ndiyo sahihi na upande mwingine siyo sahihi kabisa.
Kocha.