#SheriaYaLeo (141/366); Wajue sitaki nataka.

Kuna watu ambao kwa nje wanajifanya kama hawakitaki kitu, ila kwa ndani wanakitaka sana.

Kwa nje wanakikataa, ila ni kwa lengo la kuwafanya watu wawabembeleze ndiyo wakubali.

Watu hao wanakuwa wanajua tabia ya binadamu, kwamba ukionekana unataka sana kitu, watu wanakuzuia usikipate.
Au hata ukikipata basi utajenga wivu mkubwa kwa wengine.

Lakini mtu anapoonyesha kwamba hataki kitu, watu wanasukumwa kumbembeleza akubali.
Na pale anapokubali watu hao hawawi na wivu kwake maana wanaona wao ndiyo wamemshawishi.

Kuwa makini na watu wanaojifanya hawakitaki kitu kwa nje, wengi wao wanatumia hiyo kama njia ya kushawishiwa wakipate.

Na kwa upande wako, kama kuna kitu unakitaka kutoka kwa wengine, usionyeshe unakitaka sana.
Kwani kwa kufanya hivyo utaibua hisia mbalimbali kutoka kwa watu hao na watakukwamisha usikipate.
Na hata uking’ang’ana na kukipata, utaibua wivu mkubwa kwa wengine.

Sheria ya leo; Kuwa na wasiwasi zaidi na wale ambao wanaonekana hawana matamanio makubwa. Hiyo ni mbinu yao ya kuhakikisha wanapata makubwa bila kusumbuliwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji