#SheriaYaLeo (142/366); Kuridhisha kulikopitiliza.
Kuna watu ambao ni rahisi sana kukubaliana na wewe pale unapokutana nao.
Wanatabasamu sana, wana shauku kubwa na wanakuwa tayari kukusaidia kwa lolote.
Hilo linakufanya uwaone ni watu sahihi kwako na kuwakubali kwenye maisha yako.
Wanakuwa ni watu wanaokuridhisha na hivyo unawapa fursa mbalimbali kwenye maisha yako.
Ni mpaka baadaye ndiyo unakuja kuwajua kweli kwa undani, kwamba hawapo kama wanavyojionyesha kwa nje.
Wanakuwa ni watu wenye nia na hila fulani ambayo hawaionyeshi kwa nje.
Siyo watu wanaojali kuhusu wewe kama wanavyoonekana.
Bali ni watu wanaotaka kukutumia wewe kupata kile wanachotaka wao.
Wanakuwa wanajua tabia zao na jinsi zinavyowazuia wasikubalike na watu.
Hivyo kuondoa kikwazo hicho, wanaigiza kuwa ni watu wanaoridhisha.
Utawajua kwa namna ambavyo wanafanya kitu chochote kwa kupitiliza.
Kila njia wanayotumia kukuonyesha kwamba ni watu sahihi, wanafanya kwa kupitiliza.
Baadaye huwa wanachoka na maigizo hayo na kila kitu kuwa hadharani.
Au wanapokutana na ugumu au msongo wanashindwa kuhimili na kudhihirisha nia zao za ndani.
Sheria ya leo; Ulinzi bora kwako ni kuwaepuka watu ambao ni rahisi sana kukubaliana na wewe na wanaokuridhisha kupitiliza. Hali hiyo isiyo ya kawaida huwa inakuwa imeficha nia ovu nyuma yake.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji