2639; Kama watu wangesimamia maneno yao.
Leo hii ungekuwa mbali sana.
Hebu fikiria kama watu wote waliokuahidi watanunua unachouza, kama kweli wangenunua kama walivyoahidi si ungekuwa mbali sana?
Hebu kumbuka wote waliokuambia wapo pamoja na wewe na watapambana kufa na kupona wakiwa upande wako. Kama wangefanya hivyo leo si ungekuwa imara zaidi?
Sitaki uendelee kujikumbusha mengi zaidi, maana hayo machache tu yanaweza kuwa yamekupa masikitiko.
Ila naamini umeielewa dhana ninayokushirikisha hapa.
Wanaoahidi ni wengi, ila wanaotekeleza ahadi zao ni wachache.
Sasa hilo kinaweza kufanya ujisikie vibaya, uone watu hawana maana, uwachukie n.k.
Lakini hayo hayatasaidia, watu wataendelea kuwa watu na kufanya yale ambayo watu hufanya.
Na moja ya vitu ambavyo watu hufanya ni kuwa rahisi kuahidi, ila wagumu kutekeleza.
Badala ya kuangalia wengi ambao wanaahidi ila hawatekelezi, utakuwa salama na bora zaidi kama utapeleka umakini wako wote kwa wachache wanaoahidi na kutekeleza.
Kwa kwenda vizuri na hao wachache, inaweza kuwashawishi wengine wanaoahidi bila kutekeleza nao waanze kutekeleza.
Kitu kimoja muhimu cha kujikumbusha ni kwamba huwezi kubadili asili ya binadamu na huwezi kumbadili yeyote.
Hivyo badala ya kupoteza nguvu zako bure kwa mambo yaliyo nje ya uwezo wako, ziwekeze vizuri kwenye yale yaliyo kwenye uwezo wako.
Nenda na wale wachache wanaotimiza waliyoahidi. Shirikiana nao vizuri na uwashukuru kwa kujitoa kwao. Wape thamani kubwa ambayo haijawahi kupatikana mahali pengine.
Na hapo utakuwa umechochea tabia nyingine ya binadamu ifanye kazi kwa manufaa yako, wengine nao watataka kunufaika pia na hapo watalazimika kutimiza wanachoahidi.
Hatua ya kuchukua;
Katika wengi wanaokuahidi mambo mbalimbali, jua kuna wachache watakaotekeleza na wengi ambao hawatatekeleza.
Badala ya kuumizwa na kuhangaika na wengi wasiotekeleza, peleka nguvu zako zote kwa wachache wanaotekeleza.
Hao ndiyo unaoweza kuwatumia kufanya makubwa zaidi.
Tafakari;
Haina manufaa kulalamikia wengi waliokuahidi ila hawakutekeleza.
Badala yake washukuru wale wachache walioahidi na wakatekeleza.
Hao wanakutosha kufanya kitu cha tofauti.
Kocha.