2640; Kiranja mkuu wa dunia.
Ni cheo ambacho wengi wanakitaka, lakini hawawezi kukipata.
Kwa sababu cheo hicho hakipo.
Huwa tunapenda sana dunia iende vile tunavyotaka sisi.
Lakini hilo haliwezekani, halipo kabisa ndani ya uwezo wetu.
Tunataka kuwabadili watu, wawe na kufanya vile tunavyotaka sisi.
Lakini hilo haliwezekani, hata uwe na mamlaka kiasi gani, kama watu hawajaamua kubadilika ndani yao, huwezi kuwabadili.
Dunia huwa inaenda kwa mipango yake yenyewe. Haiulizi watu wala kufuata matakwa yao.
Iwapo utaondoka duniani leo, hakuna hata kitu kimoja kitakachosimama, mambo yataendelea kama kawaida.
Hivyo usijipe ukubwa na umuhimu usiokuwa nao.
Wewe jua wajibu wako na nafasi yako kisha vifanyie kazi.
Mengine yasikuhangaishe sana, maana yako nje ya uwezo wako.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapotaka dunia iende kama unavyotaka au kuwabadili watu wawe unavyotaka wewe, jikumbushe kwamba wewe siyo kiranja mkuu wa dunia.
Unaweza kuwa na nia nzuri sana, lakini kwa kilicho nje ya uwezo wako, huna namna ya kukiathiri.
Tafakari;
Huwa tunajitesa sana na vitu vilivyo nje ya uwezo wetu wakati kuna vingine vingi vilivyo ndani ya uwezo wetu ila tunavipuuza.
Usihangaike na chochote kilicho nje ya uwezo wako.
Kocha.