#SheriaYaLeo (145/366); Pesa rahisi.

Matapeli wote huwa wanajua mbinu moja ambayo inawasaidia sana kuwanasa wale wanaowalenga.
Mbinu hiyo ni kuibua tamaa kwa mtu.

Hakuna kitu kinachoibua tamaa kwa wengi kama fursa ya kupata pesa bure au kwa urahisi.
Tangu enzi na enzi, watu wamekuwa wanatapeliwa kwa mbinu hii.
Wanaonyeshwa kwamba kuna njia ya kupata pesa kirahisi bila ya kufanya kazi yoyote.

Hilo linaibua tamaa ndani yao na hatimaye wanaishia kutapeliwa.
Pamoja na maendeleo makubwa ya teknolojia, pamoja na upatikanaji mwingi wa maarifa, mpaka leo hii bado watu wanatapeliwa kwa njia hiyo.
Kwa sababu tamaa zina nguvu kubwa, ukishanasa kwenye tamaa, unapata upofu na kushindwa kuona mambo ya wazi kabisa.

Kumbuka hakuna kitu cha bure. Hivyo mtu yeyote anapokuja kwako akikueleza njia rahisi ya kupata pesa bila kufanya kazi, jua kuna namna anataka kukutapeli.
Kwa namna watu wanavyopenda pesa, unadhani hiyo njia ingekuwepo kweli na ingekuwa inafanya kazi wangekuja kukushawishi wewe?
Si wangekuwa ‘bize’ kweli kweli wakivuna mapesa hayo kiasi cha kutokuwa na muda na mambo mengine?

Sheria ya leo; Kuwa na wasiwasi na yeyote anayekuja kwako akikupa fursa ya kupata pesa kirahisi bila ya kufanya kazi yoyote. Njia zote za kupata utajiri kwa haraka na bila ya kazi ni utapeli na unayeumia ni wewe. Kucheza kamari ni ujinga wa hali ya juu, ni mchezo uliotengenezwa kwa namna ambayo mchezaji lazima apoteze. Hakuna njia za mkato kwenye mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji