2642; Njia za kukabiliana na msongo.

Kila binadamu huwa anapitia hali ya msongo kwenye maisha yake.

Hiyo inatokana na kwamba dunia huwa haiendi vile tunavyopanga sisi.
Hivyo chochote unachopanga, kuna mambo huwa yanaenda tofauti kabisa.
Mambo hayo yanayoenda tofauti ndiyo yanaleta hali ya msongo.

Kuna njia mbalimbali ambazo watu wamekuwa wanazitumia kukabiliana na hali hiyo ya msongo.
Tunaweza kuzigawa njia hizo kwenye makundi mawili.

Kundi la kwanza ni njia rahisi ila zisizo na manufaa.
Mfano kutumia vilevi, kula, kufanya mapenzi, kuperuzi mitandao, kufuatilia habari n.k.
Hizi ni njia rahisi kutumia ambazo zinaiondoa akili kwenye tatizo husika na hivyo kupunguza msongo.
Tatizo la njia hizi ni hazina manufaa na wakati mwingine kuwa na madhara kabisa. Mfano mtu kuwa mlevi au kuwa na uraibu wa vilevi.

Kundi la pili ni njia ngumu ila zenye manufaa.
Mfano kuwa na malengo makubwa zaidi, kufanya mazoezi, kujifunza vitu vipya n.k.
Hizi ni njia ambazo zinakusukuma ukue zaidi ya changamoto unayopitia na hivyo inakuwa haikupi tena msongo.
Njia hizi siyo rahisi, lakini manufaa yake huwa ni makubwa, kwani zinakuacha ukiwa bora kuliko ulivyokuwa awali.

Tuchukue mfano wa kuwa na ndoto na malengo makubwa sana.
Hapa unakuwa na ndoto kubwa mno ambazo kila mtu anaamini haziwezekani, ila wewe unaamini zinawezekana kabisa.
Unaweka malengo ya kuzifikia ndoto hizo kubwa.
Kisha unapambana na malengo hayo kila siku.
Pale unapokutana na vikwazo mbalimbali vinavyoleta msongo, unaporudi kuangalia ndoto yako kubwa, msongo huo haupati nafasi kabisa.
Yaani unakuwa na ndoto kubwa sana kiasi cha msongo kukosa nafasi kwako.

Hatua ya kuchukua;
Jitathmini ni njia zipi umekuwa unatumia kukabiliana na msongo kwenye maisha yako.
Kuanzia sasa acha kutumia njia zisizo na manufaa.
Badala yake tumia ndoto kubwa kukabiliana na msongo.
Kila unapokutana na changamoto zozote zinazokuletea msongo, angalia ndoto zako kubwa na jione kama umeshazifikia.
Msongo hauwezi kupata nafasi kwenye mazingira ya aina hiyo.

Tafakari;
Jinsi unavyokabiliana na msongo ndiyo itaamua unakua au unadumaa mbele ya msongo.
Mara zote tumia msongo kukua zaidi na siyo kudumaa.

Kocha.