2643; Inategemea na ngazi uliyopo.

Huioni dunia jinsi ilivyo, bali unaiona dunia kwa namna ulivyo wewe.
Unavyoiona dunia siyo uhalisia, bali ni namna mtazamo wako ulivyo.

Ukiwa masikini unaiona dunia kwa namna fulani.
Na ukiwa tajiri unaiona dunia kwa namna nyingine tofauti zaidi.
Ukiwa masikini unaikubali kila fursa inayokuja kwako, kwa sababu huna namna. Hilo linapelekea uchukue fursa ambazo siyo bora kwako na zikaishia kukutesa.
Ukiwa tajiri unakuwa na uwanja mpana wa kuchagua fursa zipi ujihusishe nazo, na hivyo kuweza kuchagua fursa bora zaidi.

Kadhalika ukiwa umefanikiwa unavyoiona dunia ni tofauti kabisa na ukiwa hujafanikiwa.
Kabla hujafanikiwa unajali sana watu wanakuchukuliaje na hivyo unafanya vitu kuwaridhisha wengine, kitu kinachokuzuia zaidi kufanikiwa.
Lakini ukiwa umefanikiwa hujali sana watu wanakuchukuliaje, kwa sababu unajua hilo halina athari kwenye mafanikio yako, kitu kinachofanya ufanikiwe zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Jiweke kwenye ngazi ya juu kabisa kifikra na kimtazamo hata kama bado hujafika kwenye ngazi hiyo kiuhalisia. Hilo litabadili sana jinsi unavyoiona dunia na jinsi unavyofanya mambo yako.
Jione kama umeshafika ngazi unayotaka kufikia, kisha katika kila maamuzi unayofanya jiulize mtu aliye kwenye ngazi hiyo anafanyaje.
Fanya kwa viwango hivyo hivyo.
Hilo linaweza kukukosesha baadhi ya fursa, lakini jua ni fursa ambazo siyo bora kabisa kwako.

Tafakari;
Kuna ushauri maarufu wa ‘fake it till you make it’. Ukiwa na maana uigize kile unachotaka mpaka utakapokipata. Ni ushauri ambao wengi huupinga kwamba siyo sahihi.
Lakini ambacho hawaoni ni kwamba ushauri huo unasaidia sana kujenga mtazamo sahihi.
Na mtazamo ndiyo kila kitu kwenye maisha.
Hivyo kama huna, igiza mpaka upate.

Kocha.