2644; Hizo nguvu hazitumiki vizuri.

Kanuni za fizikia ni kanuni za asili, hakuna namna unaweza kuzivunja.

Moja ya kanuni za fizikia ni ile ya nguvu au nishati.
Ambayo inasema huwezi kutengeneza au kuharibu nishati, bali unaweza kuibadili kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine.

Unapowasha mkaa, nguvu ya kemikali iliyo ndani yake inabadilika na kuwa nguvu ya joto.

Kanuni hiyo pia inafanya kazi kwenye nguvu za watu.
Unapoona mtu anafanya mambo ya hovyo, kama kugombana, kupigana na kutumia vilevi kupitiliza, jua ndani yake kuna nguvu ambazo hazitumiki vizuri.

Kama mtu huyo angeweza kuhamisha nguvu hizo na kupeleka kwenye kazi au mambo mengine yenye manufaa, angepiga hatua kubwa.

Nguvu za mwili huwa haziwezi kukaa tu bila kutumika.
Ndiyo maana mtu hata kama hana kazi ya maana, bado ataimaliza siku yake akiwa amechoka.

Hiyo ni kwa sababu nguvu zilizo ndani yake zitamsukuma afanye chochote kile, hata kama hakina manufaa yoyote. Maana nguvu hizo huwa haziwezi kutulia tu.

Hatua ya kuchukua;
Weka utaratibu wa kuitathmini kila siku unayoimaliza. Pale unapoona umemaliza siku ukiwa umechoka ila hakuna kubwa ulilofanya, jua nguvu zako hazitumiki vizuri.
Orodhesha yale yote unayokuwa umefanya kwenye siku yako kisha angalia yapi yasiyokuwa na manufaa.
Yaondoe hayo na weka yenye manufaa.
Mfano kama ulitumia muda mwingi kuperuzi mitandao, badili muda huo utumie kujifunza, au kuwasiliana na wateja wako, au kuzalisha zaidi.
Hakikisha nguvu zako zinakwenda kwenye mambo yenye tija kwako.

Tafakari;
Nguvu huwa haziwezi kutulia, lazima tu zitatumika. Fuatilia namna nguvu zako zinatumika ili uweze kuzipeleka kwenye mambo yenye tija kwako.

Kocha.