2645; Mstari ni mwembamba sana.

Kuna mstari mwembamba sana kati ya ushujaa na utapeli.
Kadhalika katika ya kufanikiwa na kushindwa, mshari ni mwembamba sana.

Elon Musk huwa anasema ilikuwa imebaki siku moja tu kampuni yake ya Tesla ifilisike.
Kampuni ilikuwa inahitaji sana fedha na hakukuwa na aliyekuwa tayari kuwezeka kwenye kampuni hiyo.
Ni mpaka siku ya mwisho kabisa, akiendelea kupambana ndiyo aliweza kupata fedha na kampuni ikanusurika kufa.
Hiyo ina maana kwamba mafanikio au kushindwa kwa Tesla kulitenganishwa na siku moja tu.
Ina maana kama matokeo yasingepatikana kwenye siku hiyo moja, kampuni ingefilisika na huenda leo isingekuwepo.

Ili kufanikiwa kwenye jambo lolote lile, ni lazima ujiamini kupitiliza.
Lazima uwaahidi watu mambo makubwa ambayo huna hata uhakika nayo.
Ndani yako ukijua utapambana kwa kila namna kutimiza ahadi ulizotoa.

Lakini inaweza kutokea mambo yakaenda kinyume na ulivyotegemea, yakawa nje kabisa ya uwezo wako.
Bila kujali unajiamini kiasi gani, matokeo yakawa tu ni ya tofauti.

Hapo sasa ndiyo unaonekana tapeli. Maana kwa kauli zako za kujiamini na ahadi zako kubwa, ukija kulinganisha na matokeo unayopata vinakuwa haviendani kabisa.

Lakini pale mambo yanapokwenda vizuri na juhudi unazoweka zikalete matokeo mazuri, hapo unaonekana wewe ni shujaa.
Unaonekana una akili na unaweza kuona mazuri ha mbele.

Mchakato upo kwenye uwezo wako, matokeo yako nje ya uwezo wako kabisa.
Hivyo kwa chochote unachofanya, jiamini, ahidi, kisha kaa kwenye mchakato sahihi.
Hata pale matokeo yanapokuja tofauti usiyumbishe imani yako au ahadi zako, badala yake endelea kukaa kwenye mchakato sahihi.

Unaweza kukutana na magumu na kushindwa.
Lakini kitendo cha kubaki kwenye mchakato sahihi, kitatengeneza fursa nzuri zaidi mbele.
Hata watu wengine watakuamini kwa mchakato wako, hata kama matokeo ni tofauti.

Hatua za kuchukua;
Mara zote kaa kwenye mchakato sahihi, usiruhusu chochote kukuvuruga na kukuondoa kwenye mchakato huo.
Unaweza kukutana magumu na matokeo yakawa tofauti na ulivyotegemea, usikubali kukatishwa tamaa na hayo.
Endelea kukaa kwenye mchakato.

Tafakari;
Wanasema wafu huwa hawaandiki historia. Tunasoma historia za wale waliopona, ila wapo wengi waliokufa kwa kutumia mbinu hizo hizo walizotumia waliopona.
Jua mstari uliopo kati ya kushinda na kushindwa ni mwembamba sana.

Kocha.