#SheriaYaLeo (149/366); Ukweli halisi.

Watu wapo tayari kusema chochote ili tu kutetea na kuhalalisha matendo yao.
Watatoa sababu na hadithi za kila aina kuonyesha kwamba matendo yao ni sahihi, muhimu na yenye manufaa kwa wengine.

Kwa kuwasikiliza watu, unaweza kuwaamini kwa yale wanayosema, maana wanakuwa wamejipanga vizuri kweli.
Lakini huwezi kuujua ukweli halisi kwa kuwasikiliza watu kile wanachosema.

Njia pekee ya kujua ukweli halisi ni kuangalia matendo ambayo watu wanafanya.
Na siyo tu kuishia hapo, bali kuangalia matokeo ya matendo hayo.

Matokeo ambayo watu wanayapata kwenye kile wanachofanya, ndiyo nia yao halisi ya kufanya kitu hicho.
Maelezo wanayotoa ni ya kuwahadaa tu watu wasijue nia zao halisi.

Wale wanaotaka madaraka na kutawala wengine huwa wana maneno mazuri ya kuonyesha kwamba yote wanayofanya ni kwa ajili ya wengine.
Hupenda sana kutumia neno wanyonge, kwamba wao ni watetezi wa wanyonge.

Lakini unapoangalia yale wanayofanya na matokeo wanayopata, unajionea wazi jinsi ambavyo wanajiweka kwenye nafasi ya madaraka na mamlaka makubwa zaidi.

Sheria ya leo; Wahukumu watu kwa matokeo ya matendo yao na siyo maelezo na hadithi wanazokupa. Maelezo mengi ni ya kuficha nia yao halisi, lakini matokeo yanaweka hilo wazi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji