2647; Sheria zipo wazi? Na je zinasimamiwa?
Changamoto nyingi kwenye maisha, kuanzia kwetu binafsi na hata kwa wale tunaoshirikiana nao zinatokana na sababu kubwa mbili.
Moja ni kutokuwa na sheria zilizo wazi na kujulikana na kila mmoja.
Mbili ni kushindwa kusimamia sheria hizo mara zote.
Tukianza na sababu ya kwanza, pale unapokuwa huna sheria unazozifuata kwenye mambo mbalimbali, unajikuta ukiendeshwa zaidi na hisia kuliko mantiki.
Pale jambo linapotokea na ndiyo inabidi ufanye maamuzi, kukosa sheria unazosimamia kunafanya maamuzi hayo kuwa magumu.
Na kwa sababu wakati huo hisia zinakuwa juu, basi unaishia kufanya maamuzi ya hisia.
Kuepuka hili unapaswa kujitengenezea sheria zako kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako.
Kuanzia maisha binafsi, matumizi ya muda wako na fedha zako.
Pia katika mahusiano yako na wengine na kwenye kazi au biashara zako.
Kuwa na sheria utakazozifuata wakati wote wa kufanya maamuzi.
Kwa sababu ya pili, unaweza kuwa na sheria, lakini usizisimamie, na hapo matatizo yakajitengeneza.
Unapojiwekea sheria kuna ukomo utakaotengenezwa na sheria hizo.
Utapata ushawishi wa kutofuata sheria hizo kwa sababu hutaki ukomo.
Na hapo ndipo shida zinapoanzia, kwani unaposhindwa kuzisimamia sheria hizo matatizo mbalimbali huzaliwa.
Na ubaya ni ukishavunja sheria mara moja, utashawishika kuvunja tena na tena na tena.
Kuepuka hilo hakikisha mara zote unasimamia sheria ulizojiwekea.
Unaweza kuona ni ugumu kufuata sheria zako kuliko kufanya tu kile unachojisikia, lakini jua matatizo utakayotengeneza yatakusumbua sana.
Hatua ya kuchukua;
Ni sheria zipi umejiwekea kwenye maisha yako, mahusiano, kazi, biashara na maeneo mengine?
Mambo gani hayakubaliki kabisa kwako?
Vitu gani unafanya na vitu gani hufanyi?
Ukishakuwa na sheria hizo kwenye maisha yako, zisimamie kwa gharama yoyote ile.
Hata kama unaona ni rahisi kufanya kama hutafuata sheria, usifanye, simamia sheria zako muda wote.
Tafakari;
Sheria zinatengenezwa wakati wa utulivu ili kumsaidia mtu wakati wa changamoto au machafuko.
Ni muhimu sana uwe na sheria kwenye kila eneo la maisha yako na kuzifuata wakati wote.
Hata pale unaposhawishika unaweza kunufaika zaidi kwa kutokufuata sheria zako, usifanye hivyo.
Kocha.