2648; Kama inabidi uwatishie siyo sahihi kwako.

Kama inabidi uwatishie watu ndiyo wafanye kile wanachopaswa kufanya, basi jua hao siyo watu sahihi kwako.

Kama umempa mtu kazi, lakini haifanyi mpaka umtishie kumfukuza au kutokumlipa siyo mtu sahihi kwako.

Kama kuna mtu unashirikiana naye, lakini hatekelezi wajibu wake mpaka umlazimishe au kumtishia siyo sahihi kwako kushirikiana naye.

Hata kwa upande wa wenza, kama mwenza wako hawezi kukubaliana na wewe mpaka umlazimishe au kumtishia kwa namna fulani basi siyo sahihi kwako.

Kwa nini watu hao wanakuwa siyo sahihi?

Iko hivi, hii safari ya mafanikio ni ndefu na ngumu.
Inakuhitaji uwekeze rasilimali mali zako nyingi kwenye hii safari.
Muda na nguvu zako zote zinapaswa kuwa kwenye safari hii na siyo pengine.

Sasa unapokuwa na watu ambao inabidi uwasukume na kuwalazimisha wafanye yale wanayopaswa kufanya, ni matumizi mabaya ya rasilimali zako.
Badala ya kupeleka nguvu na muda kwenye mambo yenye tija, wewe unavipoteza kwa watu ambao hawawezi hata kufanya kile wanachopaswa kufanya.

Badala ya kusonga mbele kwa kasi kubwa, unaishia kuvutwa nyuma na wale ambao inabidi uwavute kwenda mbele.

Kwa hii dunia yenye watu zaidi ya bilioni 7, usikubali kukaa na watu wanaokuwa mzigo kwako.
Unataka mafanikio makubwa, unahitaji kushirikiana na watu wanaoweza kufanya wanayopaswa kufanya bila ya kusukumwa.

Hatua ya kuchukua;
Pitia watu wote ambao unashirikiana nao kwa namna mbalimbali.
Angalia ni wapi ambao huwa wanafanya mambo yao bila ya kusukumwa, hao ndiyo wazuri kuendelea nao.
Angalia ni wapi ambao huwa hawafanyi mambo yao mpaka wasukumwe.
Nao ni wa kuwaondoa na kutafuta walio sahihi wa kuchukua nafasi zao.

Tafakari;
Muda wako na nguvu zako ni rasilimali muhimu na zenye ukomo.
Usizipoteze kwa mambo yasiyo na tija kama kulazimisha watu wafanya yale wanayopaswa kufanya.
Kwa kuwa watu huwa hawabadiliki, kila siku utajichosha huku ukishindwa kupiga hatua kubwa.

Kocha.