#SheriaYaLeo (153/366); Vaa barakoa sahihi.
Kwenye safari ya mafanikio na maisha kwa ujumla, unahitaji kubadilika ili kuendana na hali na watu mbalimbali.
Ili uweze kuwashawishi watu, inabidi uendane nao kwa namna fulani.
Na hapo ndipo uvaaji wa barakoa unapokuja.
Hapa haimaanishi kuvaa barakoa tulizozoea za kujikinga na magonjwa.
Bali inamaanisha kubadili mwonekano wako kulingana na wale unaokabiliana nao.
Unapaswa kuwa na mwonekano wenye ushawishi kwa wengine kukubaliana na wewe.
Na pia kuhakikisha watu hawajui nia yako halisi ya ndani.
Wewe wajibu wako ni kuwanasa watu wakubaliane na wewe.
Hivyo unapaswa kutumia kila njia kuwezesha hilo.
Using’ang’ane kubaki vile ulivyo mara zote, utayakosa mengi mazuri kwa kufanya hivyo.
Badala yake badilika kulingana na hali na watu.
Kwa kuwa watu ni wabinafsi, hawajali kuhusu wewe ila wanajali kuhusu wao wenyewe, unapobadilika na kuonekana kujali kuhusu wao, unajenga ushawishi mkubwa kwako.
Kubadilika kulingana na hali siyo unafiki au hadaa. Bali ni kuhakikisha unapata kile unachotaka kwenye hii dunia inayojaribu kukuzuia kwa kila namna usipate unachotaka.
Sheria ya leo; Kuweza kubadili mwonekano ili kuendana na hali na watu mbalimbali ni hitaji muhimu kwenye safari ya mafanikio na maisha kwa ujumla. Ni hitaji muhimu sana kwenye kupata na kutunza mamlaka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji