2653; Kukosoa ni rahisi, kufanya ni ngumu.
Nilikutana na hii habari mahali, kwamba waziri mkuu wa Tanzania anashangaa kwa nini nchi ina wachambuzi wengi wa mchezo wa mpira wa miguu, ambao wanaweza kukosoa mpaka makocha wa nje ya nchi, ila haina hata kocha mmoja anayefundisha nje ya nchi!
Jibu rahisi kabisa kwenye hilo ni kwamba kukosoa ni rahisi, lakini kufanya ni ngumu sana.
Kukosoa hakuhitaji juhudi yoyote, ni kufungua tu mdomo na kutema chochote kilichopo.
Lakini kufanya kunahitaji juhudi kubwa sana, kuanzia kwenye kuamua, kupanga na kutekeleza.
Kukosoa hakunaga kukosea, maana kila mtu anatoa maoni yake, kwa namna anavyoona inafaa.
Lakini kufanya mara zote huwa kuna kukosea, maana unaweza kupanga mambo yako vizuri, ila kinachokuja kutokea ni tofauti kabisa na mipango yako.
Kila aliyefanya jambo lolote kubwa hapa duniani, alikuwa na wakosoaji wengi.
Lakini leo tunawajua wale waliofanya makubwa na hatuwajui waliokuwa wanawakosoa.
Hatua ya kuchukua;
Wapuuze wakosoaji ambao siyo wafanyaji. Hakuna chochote wanachoweza kukusaidia nacho, kwa sababu kukosoa ni rahisi kuliko kufanya.
Kama mtu hajawahi kukifanya kitu kwa ubora wa hali ya juu kabisa, chochote anachokuambia kuhusu kufanya kitu hicho ni maoni yake tu. Na maoni siyo ukweli, bali ni msukumo wa hisia anazokuwa nazo mtu.
Na kama kweli unajua unachokifanya, kila ambacho wakosoaji wanakuambia tayari utakuwa unakijua, hakuna jipya wanalokuja nalo kwako, hivyo wasikubabaishe kwa namna yoyote ile.
Tafakari;
Wakosoaji ni wengi kuliko wafanyaji, kwa sababu ukosoaji ni rahisi kuliko ufanyaji.
Huna chochote cha kujifunza kwa mkosoaji asiye mfanyaji, hivyo wapuuze kabisa na peleka nguvu zako kwenye kuwa bora zaidi.
Kama unajiambia labda kuna kitu naweza kujifunza kwao, hicho ni kiashiria kwamba hujui unachofanya na hivyo mafanikio kwako yatabaki kuwa ndoto.
Kocha.