#SheriaYaLeo (158/366); Igiza nafasi yako vizuri.

Maisha ni maigizo, kile ambacho watu wanaonyesha kwa nje, sivyo walivyo ndani yao.
Hivyo moja ya wajibu wako mkubwa kwenye maisha ni kuigiza nafasi yako vizuri.

Hasa kwenye eneo la hisia, lazima uweze kuvaa hisia sahihi kwa wakati sahihi.
Pale unapohitajika kuwa na hisia za furaha uweze kuziigiza hata kama ndani yako huna furaha.
Na pale unapohitajika kuwa na hisia za huzuni uweze kuziigiza hata kama ndani yako huna huzuni.

Uzuri ni kwamba unao udhibiti wa yote hayo.
Unao uwezo wa kuigiza furaha kwa kutabasamu au kuigiza huzuni kwa kununa.
Ni muhimu sana utumie uwezo huo ili kuweza kuendana na wengine katika hali mbalimbali.

Maana ukisema uwe vile ulivyo katika kila hali, utaishia kuwaudhi watu wengi na hilo kuwa kikwazo kwako kupata unachotaka.

Kumbuka huu siyo unafiki wala ulaghai, bali ndivyo uhalisia wa maisha ulivyo. Kupata kile unachotaka lazima uweze kuendana na wengine, hata kama ndani yako unajisikia tofauti.

Kwenye kila hali unayopitia, jua ni hisia gani unapaswa kuwa nazo katika hali hiyo na kisha ziigize hisia hizo kwa uhakika wa hali ya juu kabisa.
Lakini pia usisahau upo kwenye maigizo, hivyo usiende mbali sana mpaka kujikuta na wewe umezama kwenye kile unachoigiza.

Kuigiza hakukusaidii tu kuwashawishi watu, pali pia kunawazuia wasianze kukuchunguza kwa undani na kugundua nia yako halisi kisha kuwa kikwazo.

Sheria ya leo; Kila mtu ni mwigizaji kwenye hii sinema ya maisha. Kadiri unavyoigiza nafasi yako vizuri na kuvaa barakoa sahihi kwako ndivyo unavyopata mamlaka zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji