#SheriaYaLeo (159/366); Usidharau akili za wengine.
Huwa hatupendi kukubali kwamba wengine wana akili kuliko sisi.
Tunapokutana na watu wenye akili sana, huwa tunatafuta kila njia ya kujitetea ili kuonyesha kwamba hatupo nyuma.
Tutasema wana akili za darasani tu. Au wana akili kwa sababu walisoma shule za gharama kubwa. Au wana akili kwenye lile eneo walilobobea tu.
Tunaweza kutoa kila aina ya sababu kuonyesha kwamba hatujazidiwa akili na wengine, lakini hilo halina msaada kwetu.
Kudharau akili za wengine haina manufaa yoyote kwako, zaidi ya kuwa kikwazo kwako katika kuwashawishi.
Kama unataka kuwashawishi watu wakubaliane na wewe au wakupe kile unachotaka, wafanye wajione wana akili kuliko wewe.
Wasifie kwa uwezo mkubwa walio nao na watataka kudhihirisha zaidi hilo kwako.
Waonyeshe unanufaika sana kupitia uwezo wao mkubwa wa kiakili na watazidi kukunufaisha.
Hakuna unachopata kwa kudharau uwezo wa wengine.
Watu wanapenda kusifiwa kwa uwezo wao mkubwa wa kiakili.
Tumia njia hiyo kujenga ushawishi mkubwa kwa wengine.
Sheria ya leo; Wafanye watu wajione wana uwezo mkubwa wa kiakili kuliko wewe. Wafanye waone unanufaika sana kupitia uwezo wao huo na hilo litawasukuma kutumia uwezo wao kukunufaisha zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji