2658; Inalipa sana.

Huu ndiyo mtego ambao umewanasa na kuwapoteza wengi kuliko kitu kingine chochote.

Kwa kuwa watu wana tamaa ya pesa, tena zinazoweza kupatikana kirahisi bila ya kufanya kazi yoyote, mtego huu umewanasa wengi mno.

Mtu anaposikia kitu fulani kinalipa sana, anaona hicho ndiyo cha kufanya maana anachoangalia yeye ni inamlipa kiasi gani.

Anachosahau kulipwa ni matokeo na kabla ya matokeo kuna mchakato.
Mchakato upo kwenye kila kitu na huwa ni mrefu kuliko watu wanavyotegemea.

Wakati wa mchakato huwa unapitia vipindi vigumu, vipindi ambavyo huoni mbele kama kuna matumaini yoyote.

Hapo ndipo inakuwa rahisi kushawishika na kingine unachoona kinalipa zaidi.
Unaenda kukianza, unaweka nguvu zako tena huko na kufika katikati ya mchakato kwenye ugumu.

Usipokuwa makini utajikuta kila wakati unaanza kitu kipya kwa kuona kinalipa zaidi kuliko kile unachofanya.

Ukweli ni kwamba kila kitu kinalipa, kila kitu.
Lakini kabla hujafika kwenye huko kulipa, lazima kwanza upitie hatua ambayo kitu kinakuwa kigumu na hakilipi kama ulivyotegemea.
Utayapata malipo hayo kama utaweza kuvuka ugumu huo.

Kwa bahati mbaya sana, huo ndiyo wakati wengi huacha kitu na kwenda kuanza kipya.
Hivyo kila wakati kuwa watu wa kuanza vitu vipya na kuishia njiani.

Hatua ya kuchukua;
Hicho unachofanya sasa hivi ndiyo kitu kinacholipa zaidi. Funga masikio yako pale watu wanapokuja kukuambia kuna vitu vingine vinalipa zaidi. Wewe weka mchakato wako kwenye hicho unachofanya na jipe muda wa kuvuka kipindi kigumu, baadaye utayafurahia matunda mazuri.

Tafakari;
Kila kitu kinalipa kwa namna yake ya kipekee. Usidanganyike wala kuhadaika na wale wanaokuja kwako na vitu vipya kila wakati. Weka juhudi zako kwenye kitu kimoja mpaka kikulipe kweli.

Kocha.