#SheriaYaLeo (165/366); Ongoza ukiwa mbele.
Unapokuwa kiongozi, unahitaji kuwa na ushawishi mkubwa kwa wale unaowaongoza ili wafanye yale wanayopaswa kufanyika.
Huwezi kupata ushawishi huo kwa kulazimisha au kubembeleza. Hizo ni njia zenye matokeo ya muda mfupi ila siyo endelevu.
Njia bora ya kuwa na ushawishi kwa wale unaowaongoza ni kuwa mfano halisi.
Kile unachotaka wao wafanye, anza kufanya wewe kwanza.
Viwango ambavyo unataka wafikie, anza kujiwekea wewe mwenyewe kwanza.
Kwa wale unaowaongoza kukuona ukiwa mstari wa mbele kwenye kile unachosimamia, wao wenyewe wanasukumwa kufanya ili waweze kwenda sawa na wewe.
Kuwa mfano halisi wa kile unachotaka kwa wengine na wao hawatakuwa na namna bali kufuata mfano wako.
Hamasa na morali ni ambavyo vinaambukizwa.
Ni rahisi kuwaambukiza wengine hamasa uliyonayo kuliko kuibua hamasa kwao kwa maneno au vitisho.
Kuwataka watu wafanye vitu ambavyo wewe mwenyewe hufanyi inawachosha. Wanakuwa na kila sababu kwa nini haiwezekani au hawawezi kufanya.
Lakini pale wewe mwenyewe unapokuwa mstari wa mbele kwenye kufanya, watu wanakosa sababu na hivyo kulazimika kufanya.
Kutaka kumridhisha kila mtu kwa kuacha afanye vile anavyotaka wewe kinaishia kutengeneza watu dhaifu wasioweza kukabiliana na magumu.
Jiwekee viwango vya juu, ishi viwango hivyo kwa mfano na wale wanaokufuata hawatakuwa na budi bali kuishi kwa viwango hivyo pia.
Sheria ya leo; Katika kujenga ushawishi na kupata mamlaka, unahitaji sana watu wanaokuamini na kukufuata. Watu hao wanajengwa zaidi na mfano unaoonyesha kuliko maneno au vitu vingine unavyoweza kutumia. Kuwa mfano mzuri kwa kila unalotaka kwa wengine na itakuwa rahisi kwao kufanya.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji