2665; Unahitaji watu wa kukusukuma.

Pamoja na magumu na changamoto mbalimbali za dunia, bado asili ya binadamu huwa ina nguvu sana.

Kwa mfano, ni asili yetu binadamu kuridhika na kile ambacho tayari tumeshakipata.
Pamoja na kwamba dunia inabadilika na chochote kinachoturidhisha sasa hakiwezi kuturidhisha kesho, bado hatuwezi kulivuka hilo peke yetu.

Na wala huwa hatujiambii kwamba tumeridhika, badala yake huwa tunatafuta sababu na visingizio mbalimbali vya kuturidhisha.

Mfano kujiambia hatuna muda, au hatujui au hatuna watu sahihi.
Pale unapokuwa huna msukumo mkubwa wa kufanya kitu, hukosi sababu za kujiridhisha kwa nini hukifanyi.

Kutokana na asili hiyo ya binadamu, ni vigumu sana kufanikiwa ukiwa peke yako.
Maana huwa wanasema hakuna mtu rahisi kumdanganya kama wewe mwenyewe.

Hivyo unahitaji kuwa na watu wanaokuwajibisha, watu ambao hawasikilizi sababu wala visingizio vyako. Unahitaji watu ambao watakusukuma upige hatua zaidi ya ambavyo umeshapiga mpaka sasa.

Watu hao hawapaswi kukuonea huruma kwa namna yoyote ile.
Bali wanataka uwaonyeshe matokeo.
Kwa kuwa umeahidi mwenyewe, ni lazima ufanye.

Ukiwa peke yako, ahadi zako unazichukulia kama utani tu, hujisukumi kuzitimiza.
Lakini unapokuwa na wengine, ahadi zako ni kitu unachokipa uzito mkubwa.

Unahitaji wengine wakusukume, lakini pia na wewe unahitaji kuwasukuma wengine ili wafanye makubwa zaidi.
Unahitaji watu wa kukupa changamoto ili uweze kuwa bora zaidi.

Hii safari ya mafanikio, peke yako ni ngumu sana.
Kuwa na watu sahihi wa kuambatana nao ili uweze kufika kule unakotaka kufika.

Uzuri kwenye KISIMA CHA MAARIFA tayari unayo hiyo fursa kupitia klabu za KISIMA CHA MAARIFA.
Hakikisha unakuwa kwenye klabu na unaitumia klabu vyema katika kufikia mafanikio yako makubwa na pia kuwawezesha wengine kufikia mafanikio yao makubwa.

Hatua za kuchukua;
Hakikisha upo kwenye kikundi kinachokusukuma kuwa bora zaidi.
Kikundi ambacho hakikuonei huruma au kudanganyika na sababu unazojipa.
Na wewe pia kua kiungo muhimu kwenye kikubdi hicho ili kuwasaidia wengine kupiga hatua.

Tafakari;
Raisi ana baraza la mawaziri na anawajibika kwa bunge.
Wakurugenzi wakuu wa makampuni huwa wana bodi ya wakurugenzi ambayo ina wawajibisha.
Halafu wewe unataka utoboe peke yako?
Acha kujidanganya, zungukwa na watu sahihi wanaokusukuma utoke kwenye mazoea yako na ufanye makubwa.

Kocha.