#SheriaYaLeo (170/366); Usifanye mabadiliko makubwa kwa wakati mmoja.

Sisi binadamu huwa tunapenda kusikia kuhusu mabadiliko, ila huwa hatupo tayari kubadilika.

Watu wanajua kabisa umuhimu wa mabadiliko kwenye taasisi na hata mtu mmoja mmoja.
Lakini pale mabadiliko hayo yanapowahusu wao binafsi na kuathiri maslahi yao huwa hawayafurahii.

Mabadiliko ni mazuri na muhimu, kwani yanaondoa mazoea na kuleta upya ambao unakuwa na msukumo zaidi kwa watu.
Lakini pale msukumo huo wa upya unapoisha na mabadiliko kutaka watu waweke jitihada zaidi ndipo watu wanakuwa hawapo tayari.

Hakuna mapinduzi ambayo yamewahi kwenda bila ya kupata upinzani baadaye.
Watu wale wale waliokuwa wanayafurahia mapinduzi na mabadiliko wakati yanaanza, ndiyo hao hao wanayapinga pale yanapowataka wao kubadilika.

Kuepusha hali hiyo isiwe kikwazo kwako, usifanye mabadiliko makubwa kwa wakati mmoja.
Hubiri kuhusu mabadiliko kadiri uwezavyo, lakini katika kutekeleza mabadiliko hayo nenda kwa hatua ndogo ndogo.
Na pia wakati unafanyia kazi mabadiliko, wafanye watu waone bado wanaendelea na utamaduni wao waliouzoea.

Sheria ya leo; Katika kujenga mamlaka, jionyeshe kwamba unaheshimu tamaduni zilizozoeleka. Kama mabadiliko ni muhimu, yafanye yaonekane ni maboresho ya kile kilichozoeleka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji