2668; Haya mambo huwezi kuyalazimisha.
Kuna vitu vingi unajifunza kuhusu mafanikio, lakini kina unapojaribu kuviishi unashindwa.
Labda umejifunza umuhimu wa kutumia muda wako vizuri na kutokuupoteza kwenye mambo yasiyo na tija.
Unajaribu kuzingatia hilo ila bado unajikuta tu unapoteza muda kwa mambo yasiyo na tija.
Labda umejifunza kwamba kuongea sana kuyafanya udharaulike, unapanga usiwe mwongeaji sana.
Lakini unajikuta tu umeshaongea sana.
Na mengine mengi unauojifunza, kila unapojaribu kuyatekeleza unashindwa.
Na hapo unaweza kudhani labda wewe una matatizo, kwa nini mambo hayo hayawezekani kwako?
Leo nataka nikutoe hofu, siyo kwamba una tatizo, ila tu ni kwamba hayo mambo mengi unayojifunza huwezi kuyaiga wala kuyalazimisha.
Huwa yanatokea tu yenyewe baada ya wewe kujiweka kwenye mchakato fulani.
Kwa mfano kwenye muda, utakapoanza kutoa thamani kubwa zaidi kupitia kile unachofanya, wengi zaidi watataka kufanya kazi na wewe au kununua kwako.
Na hapo moja kwa moja unajikuta muda haukutoshi, hivyo njia pekee inakuwa kuacha mambo yasiyo na tija.
Ukienda kwenye kutokuongea sana, unapojifunza kwa kina kuhusu mambo mbalimbali, ndivyo unavyoona ni kwa kiasi gani usivyojua mambo mengi.
Moja kwa moja unajikuta hutaki kuongea sana kwa sababu unajua hujui na unajua hao wengine pia hawajui na ukijaribu kuwaeleza watakuwa wabishi. Hapo unakuwa huna namna bali kukaa kimya.
Ukishajiona tu unahangaika kuiga au kulazimisha vitu fulani, jua kuna hatua umeiruka. Rudi kwanza kwenye hatua hiyo na hutahitaji kuiga au kulazimisha chochote, mambo tu yatatokea yenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Orodhesha vitu vyote ambavyo umekuwa unajaribu sana kufanya lakini unashindwa.
Kwa kila ulichoorodhesha jiulize ni hatua ipi uliyoiruka.
Rudi kwenye hatua hiyo na kile unachotaka kitawezekana.
Tafakari;
Ukiwa na njaa hujilazimishi kula.
Ukiwa na kiu huigizi kunywa maji.
Ukiwa unaumwa sindano haiumi sana.
Kila kitu kina mahitaji yako ili kiweze kufanyika.
Kama unalazimisha kuna hatua ambazo zimerukwa.
Kocha.