2669; Nini ni sahihi na siyo nani yuko sahihi.
Changamoto kubwa tunazokutana nazo kwenye maisha huwa zinaanzia kwenye hukumu tunazotoa kwa wengine.
Mara nyingi hukumu hizo huwa ni za upendeleo.
Kama mtu tunampenda au kukubaliana naye tunamhukumu vizuri kwa sababu tunaona upande wake mzuri tu.
Na kama mtu hatumpendi au kukubaliana naye tunamhukumu vibaya kwa sababu tunaona upande wake mbaya tu.
Tukishawahukumu watu ndiyo tunawachukulia hivyo.
Hatuwi tayari kubadilika hata pale watu hao wanapobadilika au tunapopata taarifa zaidi kuwahusu.
Kuwahukumu watu ni kujinyima fursa ya kuujua ukweli.
Kama unataka kuujua ukweli, usihangaike sana na watu, bali hangaika na mambo.
Badala ya kuangalia nani yupo sahihi au hayupo sahihi, angalia nini kipo sahihi.
Kwa kuangalia watu, hisia zetu zinatuingilia na kushindwa kufanya maamuzi sahihi.
Kwa kuangalia hali au mawazo, tunaweza kuweka hisia zetu pembeni na kuamua vyema.
Ni muhimu pia kuepuka itikadi, maana hizo nazo huwa hazina kufikiri wala kudadisi, ni kupokea kitu kama kilivyo.
Ili kuupata ukweli na kuwa huru, lazima udadisi kila kitu, ukihoji na kujua ukweli wake.
Lazima uepuke sana kuhukumu mapema kabla ya kupata taarifa za kutosha.
Hatua ya kuchukua;
Katika kufanya maamuzi, usiangalie nani yupo sahihi au hayupo sahihi, badala yake angalia kipi ni sahihi au siyo sahihi.
Kwa kuangalia vitu badala ya watu, utavuka udhaifu wako wa kutekwa na hisia katika kufanya maamuzi.
Mara zote kuwa tayari kubadilika pale unapopata taarifa bora zaidi ya ulizokuwa nazo awali.
Hiyo ndiyo namna pekee ya kuwa bora zaidi.
Tafakari;
Maamuzi mengi tunayafanya tukiwa na sehemu tu ya taarifa zinazohusu hicho tunachofanyia maamuzi.
Kadiri tunavyokwenda, tunapata taarifa zaidi na hivyo tunapaswa kuendelea kuboresha maamuzi hayo.
Hilo litawezekana kama ulifanya maamuzi kulingana na hali na siyo kulingana na watu.
Kocha.