#SheriaYaLeo (174/366); Dhibiti kile unachosema.
Mamlaka ni mchezo wa mwonekano kadiri unavyozungumza kidogo, ndivyo unavyoonekana wa muhimu na mwenye mamlaka makubwa.
Unapokaa kimya unawafanya wengine washindwe kukutabiri.
Maana sisi binadamu ni mashine za kutengeneza maana, huwa hatuwezi kutulia kama hatujui maana au nia ya kitu fulani.
Unapozungumza sana, unaweka kila kitu wazi na watu wanajua maana na nia uliyonayo na hivyo wanakuona wa kawaida.
Lakini unapokaa kimya, watu wanashindwa kuelewa maana na nia uliyonayo na hivyo wanakuona wa maana zaidi.
Unapowajibu kwa ufupi wanasikiliza kwa makini na kukimbilia kuongeza maelezo zaidi, kitu kinachokupa wewe fursa ya kuwajua zaidi na kujua nia zao.
Kwa kuwa wewe huongei sana, watajikuta wao wanaongea zaidi kitu kitakachokuwezesha kujua udhaifu wao.
Wanapomaliza mazungumzo na wewe, wataondoka wakiwa wanajiona kama wameibiwa, maana wameeleza mengi ila wameondoka na machache.
Wataendelea kutafakari kwa kina kila neno ulilozungumza wakijaribu kutafuta maana na nia yako.
Na hilo litakufanya uwe na mamlaka zaidi juu yao.
Sheria ya leo; Watu wenye mamlaka makubwa huwa siyo wazungumzaji sana. Wanadhibiti sana kile wanachosema, wanasema kidogo na kukaa kimya zaidi kitu kinachowasukuma wengine kusema sana. Hilo linawapa nafasi ya kuwajua wengine kwa undani huku wao wakiwa hawatoi fursa kwa wengine kuwajua kiundani. Yote hayo yanafanya mtu awe na mamlaka zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji