#SheriaYaLeo (176/366); Tumia maneno matupu.

Watu huwa wanapenda na hata kuelewa zaidi lugha ya picha.
Hiyo ni kwa sababu inawawezesha kujenga taswira ya kitu na kukielewa vizuri.

Unapotaka kuwahadaa watu, nenda kinyume na hilo. Tumia lugha ya maneno matupu ambayo hayamwezeshi mtu kujenga taswira yoyote.

Lugha ya aina hiyo inamfanya mtu ashindwe kujua kama ni ukweli au uongo, kwa sababu hakuna picha yoyote ambayo anaipata.

Lugha unayotumia inakuwa nzuri, ya kuvutia na inayoibua hisia, lakini haisimami kwenye kitu chochote.

Hilo linafanya watu kuhadaika na lugha na kutokudadisi kama kinachosemwa ni kweli au la.

Hii ni mbinu ambayo imekuwa inatumiwa sana kwenye zama hizi za maarifa na taarifa.
Wenye hila fulani wanatoa taarifa ambazo zina ushawishi ila hazimaanishi chochote.

Ni vyema pia uwe makini na maneno unayosikia kwa wengine.
Pale unapoona maneno ni matupu, yasiyo na maana yoyote lakini yamepangiliwa vizuri kwa namna ambayo yanavutia na kuteka, jua unahadaiwa.

Sheria ya leo; Tumia maneno matupu na yanayochanganya ili watu wasiweze kujua nia yako halisi. Wateke kwa mbwembwe na hisia ili wasiweze kudadisi na kujua nini hasa unachotaka kufanya au kupata.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji