2674; Uongozi ni kuwaudhi watu kwa manufaa yao wenyewe.
Kama hutaki kuwaudhi watu.
Basi usiwe kiongozi.
Kwa sababu wajibu mkubwa wa kiongozi ni kuwafanya watu wafanye vitu ambavyo hawataki kufanya, ila vina manufaa kwao.
Yaani kitu kina manufaa kwa mtu, lakini hataki kukifanya, kwa sababu ni kipya kwake au kigumu.
Kama kiongozi unapomwezesha mtu kufanya kitu hicho na baadaye akapata matokeo mazuri, atakushukuru sana.
Lakini kabla ya kufika kwenye matokeo hayo mazuri na kukushukuru, atapitia kwanza kwenye ufanyaji mgumu na kukulaumu.
Atakuona ni mtu usiyejali wala usiyefaa.
Atakupa lawama za kila aina.
Kama hutakuwa na msimamo, utamwachia na hatapata matokeo makubwa na mazuri.
Hivyo ni wajibu wako kama kiongozi kuwashikilia watu wako kwenye kile wanachopaswa kufanya bila ya kuwa na huruma au kuwaachilia.
Na siyo kwamba unawatesa au kuwakomoa, bali unawaepusha na uvivu na uzembe ulio ndani yao.
Ili uwe kiongozi mzuri na mwenye manufaa kwa watu hupaswi kuwa mwoga.
Hupaswi kuwa mtu wa kubembeleza au kutaka kumfurahisha kila mtu.
Unapaswa kuwa na maono ya wapi unataka watu wako wafike.
Kisha ujue nini wanapaswa kufanya ili wafikie maono hayo.
Halafu unawashikilia kwenye kufanya hayo bila ya kuwaruhusu kutoroka.
Hapo ndipo ugumu ulipo, kwani watu watatengeneza kila aina ya sababu ili tu wasifanye kile wanachopaswa kufanya.
Kiongozi ukijiona una roho nzuri sana au unajali sana, utakubaliana nao na hapo ndipo unapokuwa umeharibu.
Ni lazima ushike udhibiti wa kile kinachopaswa kufanyika na kuhakikisha kinafanyika kweli.
Katika kushika udhibiti huo kuna watu utakaowaudhi.
Watakuona una roho mbaya na usiyejali.
Lakini watalazimika kufanya na hapo ndipo wataweza kupata matokeo mazuri.
Kama utataka usiwaudhi watu na ukataka umpe kila mtu kile anachotaka, utaishia kutengeneza vurugu zisizo na mfano.
Kila mtu atafanya vile anavyoona ni sahihi na hakuna yeyote atakayepata matokeo mazuri.
Kutaka kuonekana una roho nzuri kama kiongozi kunapelekea uwe kiongozi mbovu na usiyezalisha matokeo yoyote.
Jamii zetu zimekuwa laini sana kwenye zama hizi. Watu wanataka sana kupendwa na hawataki kuwaudhi wengine. Hivyo hawapo tayari kusimamia kitu kwa misingi sahihi, badala yake wanataka kumridhisha kila mtu.
Asili ya binadamu huwa haibadiliki, watu kwa asili ni wavivu na bila ya kuongozwa huishia kujipoteza wao wenyewe.
Viongozi wazuri ni wale wanaowaonyesha watu wapi wanatakiwa kufika, kuwaonyesha njia ya kufika huko kisha kuhakikisha wanakaa kwenye njia hiyo mpaka wafike wanakopaswa kufika.
Watu wanaweza wasifurahie sana safari hiyo, lakini mwisho wa safari watakurahia na kumshukuru sana kiongozi.
Bila ya uongozi imara watu hupotea na kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwao.
Chagua kuwa kiongozi, kubali kuwaudhi wengine na kulaumiwa na pambana kuwafikisha watu wako kwenye maono makubwa.
Hiyo ndiyo njia bora ya kuacha alama kwa wengine.
Hatua ya kuchukua;
Ni eneo gani la maisha yako ambalo unawaongoza wengine?
Kama bado hujatengeneza maono makubwa kwa watu wako fanya hivyo. Kama tayari jikumbushe maono hayo kila mara.
Wasukume watu wako kuweza kuyafikia maono hayo bila ya kuruhusu uvivu au uzembe wa aina yoyote ile kuwa kikwazo kwao.
Utawaudhi wakati wa safari, lakini watakuja kuyafurahia sana matokeo ya mwisho.
Tafakari;
Watu huwa ni rahisi sana kujidanganya wao wenyewe.
Hujipa sababu na visingizio visivyo na mantiki kabisa.
Kazi yako kama kiongozi ni kuwazuia watu wasijidanganye wao wenyewe.
Mwanzo hawatakuelewa, ila baadaye ndiyo wataona manufaa ya kile unachofanya.
Usiingie kwenye mtego wa watu kujidanganya kwa kutaka kuonekana unawajali.
Kuwajali kwako ni kuhakikisha wanafika kule wanakopaswa kufika.
Kocha