#SheriaYaLeo (184/366); Usiwaridhishe watu haraka.
Uwezo wa kuchelewa kuwaridhisha watu una nguvu kubwa kwenye ushawishi.
Unawajengea watu hali ya matumaini lakini pia hali ya kukuhitaji zaidi.
Ile hali ya kuonekana hutaki sana kitu au hujali sana inakupa wewe nguvu kubwa.
Kwani wengine wanasukumwa kukushawishi na kukubembeleza ili uweze kuwapa kile wanachotaka.
Lakini pale unapoonekana kuwahitaji sana watu, pale unapojali kupitiliza, watu wanakuzoea na kutokukupa uzito wowote, kitu ambacho kinapunguza ushawishi na mamlaka yako.
Kufanikisha hili lazima uonekane kuweza kujitegemea wewe binafsi bila ya uhitaji wa watu wengine.
Pale watu wanapoona huna uhitaji kwao ndiyo wanasukumwa kukutaka zaidi.
Lakini pale unapowategemea sana na kuwa na uhitaji mkubwa kwao wanakuchukulia kawaida na kutokukuhitaji.
Ni muhimu ujue nguvu ya mapenzi na tamaa, kadiri unavyowahitaji watu, ndivyo unavyowakimbiza.
Kuwapa watu umakini mkubwa huwa ina nguvu mwanzoni, lakini baadaye inazoeleka na kukosa nguvu.
Inaonyesha udhaifu na uhitaji, kitu kinachopunguza ushawishi.
Huwa tunafanya sana kosa hili, kudhani kwamba kumfuatilia sana mtu ndiyo kuwa na uhakika wa kumshawishi na kumpata.
Lakini ukweli ni kinyume chake, kadiri unavyoonekana kutokumfuatilia na kumtaka sana mtu, ndivyo mtu huyo anavutiwa zaidi kwako na inakuwa rahisi kumshawishi.
Mtu huyo ndiye anayejikuta kwenye hali ya kutokuwa na uhahika, asijue kama kuna kitu amefanya kikakuudhi. Kutokuwa kwao na uhakika ndiyo kinawafanya wao wakufuatilie zaidi na wawe tayari kushawishika na kile unachowaambia.
Kwa sababu wanataka sana uhakika wako kwao.
Sheria ya leo; Kujenga ushawishi mkubwa kwa watu, usiwaridhishe haraka. Usionekane kuwafuatilia sana au kuwahitaji kupitiliza. Waweke kwenye hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu wewe na hilo litawasukuma wakufuatilie zaidi na hivyo kushawishika na wewe zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji