2684; Kwani umefikaje kwenye hicho kilele?
Fikiria umemkuta mtu kwenye kilele cha mlima na ukamuuliza amewezaje kufika kwenye hicho kilele.
Unadhani atakuambia nilikuwa nazurura zurura tu hapo chini ya mlima na hatimaye nikajikuta nipo kileleni?
Jibu ni hapana, atakueleza wazi kwamba alipanga kupanda mlima huo, kisha akapiga hatua moja baada ya nyingine mpaka kweli akafika kwenye kilele cha mlima.
Kadhalika unapokutana na mtu ameandika kitabu na ukashangazwa amewezaje, hatakuambia alikuwa anaandika andika tu maneno kisha kitabu kikatokea.
Atakueleza wazi kwamba aliweka lengo la kuandika kitabu na akakaa chini kuandika mkapa kukamilisha.
Lakini wewe sasa, unataka kuonyesha dunia muujiza ambao haujawahi kuwepo, wa kuzurura zurura tu bila mpango wowote na mwishoni kujikuta kwenye kilele cha mlima.
Kukuambia ukweli ni unajidanganya, utapoteza muda wako na hata pamoja na kuzurura sana, bado utajikuta unaishia pale ulipoanzia.
Kwa chochote kile unachotaka kwenye maisha yako, kwanza unaweka lengo la kukifikia, kisha unaweka mpango wa namna ya kukifikia.
Halafu sasa unaweka mchakato kwenye mpango wako huo bila kuacha au kuyumbishwa na chochote.
Utauliza kwa muda gani sasa?
Na mimi nitakuuliza kwani umepanga kuacha kula chakula lini?
Unaona, kama utakuwa unakula kila siku, basi pia utapaswa kufanyia kazi malengo na mipango yako kila siku bila kukata tamaa.
Kuna neno huwa nalirudia sana na nitalisema tena hapa, ili ulisikie mpaka ligande kwenye fikra zako.
NI MCHAKATO, hakuna kingine, weka nguvu zako kwenye mchakato maana hicho ndiyo unachokidhibiti.
Usizurure zurure tu, usihangaike na yasiyokuwa na tija, weka malengo na mipango kisha kaa humo.
Itakuwa swala la muda tu kupata kile unachotaka.
Hatua ya kuchukua;
Leo jitathimi kwa maswali haya matatu muhimu, jiulize na kuandika majibu yake.
Nini hasa unachokitaka kwenye maisha yako? Ipi ndoto yako kubwa?
Ni mpango gani unaoufanyia kazi ili kufika kwenye ndoto yako?
Ni vitu gani umekuwa unafanya kila siku ili kukamilisha mpango wako na kufikia ndoto yako kuu?
Majibu ya maswali hayo yatafanya uone kama upo makini na unachotaka au unazurura tu.
Tafakari;
Yeyote unayemuona amefika mahali pakubwa zaidi, hakufika pale kwa bahati au ajali.
Bali alifika hapo kwa malengo na mipango.
Weka malengo na mipango na ukomae nayo mpaka upate kile unachotaka.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining