2685; Ni rahisi mpaka utakapoanza kufanya.
Mipango ya kitu chochote kile huwa ni rahisi sana.
Na unaweza kujionea wazi kabisa kwamba kila kitu kitakwenda sawa kabisa.
Unapoona wengine wanafanya kitu unaona ni rahisi kufanya.
Kwamba hata wewe ukiamua unaweza kufanya kama wao.
Tena unaweza kuona utafanya zaidi yao.
Ni mpaka pale unapoingia kwenye kufanya kitu ndiyo unagundua siyo rahisi kufanya kama ulivyodhani.
Ni katika kufanya ndiyo unakutana na magumu ambayo hukutegemea yangekuwepo kwenye kile unachofanya.
Hili halimaanishi uogope vitu na kutokufanya.
Badala yake inakupata ukipe kila kitu uzito ambao unastahili.
Wengi wanaingia kwenye vitu bila ya kuvipa uzito unaostahili na ndiyo maana wanaishia njiani.
Mwanzo wanakuwa wanasukumwa na hisia kuliko uhalisia.
Ni sawa na mtu anayeanza kwa kasi kubwa mbio ndefu, anachoka haraka kabla hata hajafika nusu ya mbio hizo.
Kama kuna kitu unataka kikupeleke kwenye mafanikio makubwa, jua wazi kwamba hakitakuwa rahisi.
Kitakuwa na magumu na changamoto mbalimbali.
Kitakuwa na vikwazo vya kila aina.
Lakini kama umejitoa kweli kufanya, utaendelea kufanya na hatimaye kupata matokeo makubwa.
Na kwa upande mwingine kama unachofanya ni rahisi kabisa na hakina magumu wala changamoto zozote basi huenda siyo sahihi au unafanya kwa viwango vya juu kabisa.
Kila unapojiona mambo ni rahisi na yanakwenda bila ya kukusumbua ni wakati wa kubadilika.
Ni wakati wa kuweka malengo na mipango yako upya kwa namna ambayo vinakusukuma zaidi ili uweze kufanya makubwa zaidi ya yale unayofanya.
Hatua za kuchukua;
Jikumbushe lini umekutana na ugumu kwenye kile unachofanya, ugumu uliopelekea hali ya kukata tamaa.
Kama umekutana na hali hizo karibu basi unapambana na makubwa.
Lakini kama hukumbuki umekutana na hali hizo lini, basi hupambani na chochote, unafanya ambayo hayawezi kukupa makubwa.
Tafakari;
Ukiona ni rahisi kupanga usidhani pia itakuwa rahisi kufanya.
Ukiona wengine wanafanya kwa urahisi usidhani na wewe utaweza kufanya kwa urahisi pia.
Ukiona vitu vinakwenda kwa mteremko kwako, jua kuna mahali unakosea.
Mambo makubwa hayajawahi kuwa rahisi.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining