#SheriaYaLeo (190/366); Wasioshawishika.
Katika harakati zako za kutaka kuwashawishi wengine ili wakupe kile unachotaka, utakutana na watu ambao hawawezi kushawishika.
Hawa ni watu wasiojiamini kupitiliza.
Kila mmoja wetu huwa anakuwa na hali ya kutokujiamini. Lakini katika mchakato wa ushawishi, huwa hali hiyo inavukwa kirahisi.
Kwa wasioshawishika, kutokujiamini kwao kunakuwa kumepitiliza.
Wanakuwa na mahitaji na wasiwasi mkubwa kiasi kwamba hawawezi kuingia kwenye mchakato wa ushawishi.
Ni watu wa kujihami haraka sana kwa chochote kile kinachofanyika.
Wanatafsiri kila kitu kama mashambulizi au usaliti kwao.
Huwa wanakimbilia kulalamika na kulaumu kuhusu kila kitu.
Changamoto ni kwamba watu hao siyo rahisi kuwatambua mapema.
Unaweza kuwaona wapo kawaida na wanashawishika, ila ni mpaka pale unapoingia kwenye mchakato wa kuwashawishi ndiyo unagundua siyo wa kushawishika.
Hivyo kuwatambua ni muhimu uangalie dalili zao kuu ambazo ni hali ya kutokujiamini kupitiliza, kukosa shukrani na kuwa watu wa kujitetea sana na kulaumu wengine.
Wanaweza pia kukusifia kupitiliza na kuonyesha kukupenda sana.
Wakati mwingine wanakuwa hawajali chochote kuhusu wewe.
Ni muhimu sana uwajue hao wasioshawishika ili usipoteze nguvu na muda wako bure.
Sheria ya leo; Watambue mapema wasioshawishika ili uweze kuwaepuka au kuwa na mbinu bora zaidi za kuwashawishi. Pia ondokana na tabia za kutokushawishika, kwani hutaweza kuwashawishi wengine.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji