2689; Hakuna asilimia 100.

Hakuna kitu chenye ufanisi wa asilimia 100.

Hata injini ya gari, pamoja na uwezo mkubwa ambao inakuwa nao, haifikii ufanisi wa asilimia 100.
Kuna nguvu nyingi inapotelea kwenye msuguano.

Mnyama mkali kama simba ambaye anaweza kuwadhuru karibu wanyama wengine wote wa mwituni, hana ufanisi wa asilimia 100. Katika wanyama wengi ambao atawakimbiza kwa ajili ya kupata chakula, ni wachache sana ndiyo atafanikiwa kuwakamata.

Hata biashara kubwa unazoziona na wale waliofanikiwa sana.
Siyo kwamba wanapatia mara zote.
Kuna mara nyingi sana ambazo wanakosea.
Lakini kwa sababu wanafanya mengi na kwa muda mrefu, machache yanakuwa na matokeo mazuri.

Tatizo linakuja kwako, pale unapoamini inabidi ufanye kwa asilimia 100 au bora usifanye kabisa.
Pale unapoona unapaswa kuwa na ufanisi kamili la sivyo ni bora usikaribu kabisa.
Pale unapofikiri unapaswa kufanya kwa usahihi kamili la sivyo haina haja ya kujaribu.

Rafiki, huko siyo tu kujichelewesha, lakini pia ni kujificha.
Ni kuchagua kitu ambacho hakiwezekani na kukitumia kama sababu.

Ni wakati sasa wa kuacha kujichelewesha na kujificha.
Chagua kufanya kwa namna unavyoweza kufanya.
Hata kama utafanya kwa udogo na uchache, ni bora kuliko kutokufanya kabisa.
Hata kama utaanza kwa kukosea, utajifunza mengi ambayo hukuwa unayajua.

Kama simba anaishi pamoja na kushindwa kwenye mawindo yake mengi, hebu fikiria ni hatua kubwa kiasi gani utapiga kwa kufanya bila kujali ni kiwango au usahihi kiasi gani ulionao?

Hatua ya kuchukua;
Rudi kwenye chochote ambacho umekuwa unapanga kufanya lakini unaahirisha kwa kujiona bado hujawa tayari.
Angalia nini kinakukwamisha.
Amua sasa utafanya kwa viwango vyovyote vile.
Hutaangalia ni kwa ukubwa au usahihu kiasi gani.
Wewe utafanya, kisha kujitathmini na kufanya kwa ubora zaidi.

Tafakari;
Kutaka uhakika ni kichaka ambacho wengi ambao hawajajitoa kweli kufanya huwa wanajificha.
Wewe usijifiche hapo, jua hakuna chochote duniani chenye ufanisi wa asilimia 100.
Hivyo fanya chochote unachoweza kufanya, ni bora kuliko kutokufanya kabisa.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining