2690; Tatizo siyo kujua.

Watu wengi huhangaika sana na kutafuta siri za mafanikio.
Huwa wanadhani kuna kitu kimefichwa ambacho wakishakijua tu basi mafanikio yatakuwa rahisi kwao.

Lakini huo siyo ukweli,
Ni njia tu ya watu kujificha na kuukwepa ukweli ambao upo dhahiri.

Karibu kila mtu anayetaka kufanikiwa, tayari anajua nini anapaswa kufanya ili afanikiwe.
Hilo lipo wazi kabisa.

Lakini kwa kuwa anachojua hakiendani na vile alivyodhani yeye, basi anaona siyo sahihi.
Na hapo ndipo anaanza kuhangaika na mengi yasiyokuwa na tija.

Ndiyo maana nasema tatizo siyo kujua, tatizo ni kufanyia kazi kile ambacho mtu unajua.
Hata kama unajua kiasi gani, kama hufanyii kazi hakuna kitakachobadilika.

Unayojua yatakuwa na maana kwako kama utayafanyia kazi.
Kuhangaika na kujua zaidi haitakuwa na msaada kama hata hutumii yale ambayo tayari unajua.

Sisemi mtu asiendelee kujifunza, hilo ni lazima. Ninachosema ni mtu asitumue kujifunza kama sababu ya kutokufanya.
Usijiambie huanzi mpaka ujue kitu fulani.
Tayari unajua kiasi cha kutosha kuanza, anza na kile unachojua na kadiri unavyokwenda utaendelea kujifunza zaidi na kuboresha ufanyaji wako.

Hatua ya kuchukua;
Kama ungekuwa unafanyia kazi yale yote unayoyajua mpaka sasa, ungekuwa umepiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
Habari njema ni kwamba hujachelewa, unaweza kuanza sasa na ukafanya makubwa mno.
Fanyia kazi yale ambayo tayari unayajua na utashangaa hatua utakazopiga.

Tafakari;
Kujua pekee haitoshi wewe kupata matokeo ya tofauti.
Ni lazima uchukue hatua kwenye yale unayojua.
Usitumie kutokujua kama kichaka cha kujificha.
Pamoja na kuendelea kujifunza, endelea pia kufanya kwa kutumia kile ambacho tayari unajua mpaka sasa.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining